Makala

FATAKI: Mapenzi ya kweli si tu kutembea mmeshikana mikono

March 28th, 2020 1 min read

Na PAULINE ONGAJI

[email protected]

SIKU kadhaa zilizopita nilisoma maoni fulani ya kuchekesha mtandaoni.

Maoni hayo yalikuwa yamechapishwa na binti mmoja ambapo alizungumzia hatua ya serikali kutoa amriya kutotoka nje kuanzia Ijumaa Machi 27, 2020, kati ya saa moja usiku na saa kumi na moja alfajiri.

Katika maoni hayo, binti huyo alionekana kuwadhihaki madume ambao kutokana na amri hiyo sasa wanakumbana na uhalisi mgumu wa kukaa nyumbani; na wake zao ambao wamekuwa wakiwatoroka mambo yalivyokuwa kawaida.

Kulingana na binti huyu, wanaume hawa sasa wamelazimika kukabiliana ana kwa ana na uhalisi wa kukaa nyumbani na wanawake waliooa sio kwa sababu ya mapenzi, bali ili kufuruhasisha jamaa zao na jamii kwa ujumla.

Ni kauli ninayokubaliana nayo asilimia mia fil mia, ila sio wanaume tu wanaoathirika na suala hili, kwani pia kuna wanawake walio katika mahusiano na ndoa kutokana na sababu zingine na wala sio mapenzi.

Kuna baadhi ya watu ambao mahusiano na ndoa zao zinatawaliwa na madaha ili kufurahisha jamii, huku wao wenyewe wakiendelea kuzama katika huzuni.

Nazungumzia wale wanaodhani penzi la kweli ni kushikana mikono mkiwa katika sehemu za umma, kuvalia vitenge vinavyofanana au kuanika picha zenu mkiwa pamoja, mtandaoni.

Mara nyingi vitu hivi hufumba wengi macho na kusahau machungu au hisia za kutoridhishwa katika uhusiano au ndoa kwani nia yao ni kufurahisha umma, ilhali kwa uhalisi wanaendelea kuumia.

Sio tu kwa wanaume, bali pia kwa mabinti; usioe wala kuolewa na mtu fulani eti kwa sababu ya kuwafurahisha wengine. Fanya hivyo kwa raha zako mwenyewe kwani mwishowe sio hiyo jamii itakayotarajiwa kuishi na binti au kaka huyo. Ni wewe.