Makala

FATAKI: Mume au watoto wasiwe minyororo maishani!

August 31st, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

HIVI majuzi kuna rafiki yangu aliyenisimulia kisa kilichomtendekea siku kadha zilizopita.

Kuna kaka fulani; mume wa mtu na ambaye amezoea kupiga gumzo naye kwenye WhatsApp.

Lakini mara hii alipata kaka kamblock kwenye jukwaa hili na baada ya kumpigia simu, dume hilo lilijitetea kwamba mkewe ndiye wa kulaumiwa.

“Sio mara ya kwanza kwake kufanya hivi kwani yeye huchakura simu yangu na kila anapoona gumzo na binti fulani, basi yeye humblock,” alisema.

Ni suala lililonikumbusha kisa cha miezi kadha iliyopita ambapo nilikumbana na video fulani ya zamani iliyomwonyesha mwanamke mmoja akiharibu gari la mumewe eti kwa sababu alimfumania na kipusa fulani kwenye baa.

Visa hivi vinashangaza kwamba kuna baadhi ya wanawake walio na wakati mwingi sana hadi wa kujitwika jukumu la ujasusi maishani mwa wapenzi au waume zao.

Suala hili linanikumbusha maoni yangu ya miezi michache iliyopita kuhusu hawa wanawake wanaojitia aibu au hata mashakani kwa kupigania wanaume.

Hasa nakumbuka kisa cha binti mmoja aliyemmwagia mwenziwe asidi usoni eti kwa sababu alikuwa mpenzi wa pembeni wa mumewe.

Mbali na kumuachia muathiriwa majeraha mabaya, bibi sasa anaozea korokoroni kwa kifungo cha miaka 24.

Himaya

Bila shaka suala la himaya katika uhusiano na ndoa sharti liheshimiwe, lakini matukio hayo yanadhihirisha jinsi baadhi ya mabinti miongoni mwetu hawazingatii umuhimu wa kuwa na maisha yao binafsi kando na mahusiano yao.

Mojawapo ya mambo yanayosababisha wanawake wengi kujitia aibu hivi ni kwamba wanataka kutambuliwa kama mke au mama ya fulani.

Bila shaka ni vyema kutambuliwa hivi, lakini kama mtu binafsi unajivunia nini? Kumbuka kwamba kabla ya kuwa mke au mama ulikuwa mtu fulani.

Ikiwa wewe ni mmoja wao, tafadhali jiondolee msongo wa mawazo na mfadhaiko kwa kuwa na maisha kivyako; maisha yasiyomzunguka mpenzio, mumeo au wanao.

Mara kwa mara ungana na marafiki zako kuvinjari, nenda likizoni peke yako ili kurutubisha nafsi yako. Mbali na kukusaidia, pia unapunguza uwepo wako kila mahali na hivyo kukuondolea presha.

Mpe nafasi ya kukaa na wanaume wenzake na kuburudika kwa kinywaji angalau aweze kukutamani pia.