Makala

FATAKI: Mwanamke anayejua thamani yake hawezi akavumilia kuwa 'mlo wa pembeni'

August 17th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

HIVI majuzi mojawapo ya habari zilizotawala vyombo vya habari ni vifo vya wanasiasa wawili wakuu.

Hasa kifo cha mwanasiasa wa kiume ndicho kiliibua gumzo zaidi na mwangaza mbaya, baada ya binti fulani kujitokeza na kwenda kortini ili kusimamisha shughuli za mazishi eti hadi mwanawe aliyesema kamzaa na mwanasiasa huyu atambulike.

Ni suala lililoibua mjadala hata kwenye vyombo vya habari na nakumbuka katika kituo kimoja cha redio, watu walipiga simu kutoa maoni yao.

Japo baadhi ya watu waliunga mkono hatua ya mwanamke huyu, wengi walionekana kukerwa huku wakisema kwamba kama mwanamke wa pembeni, hauna haki yoyote ya kusababisha kizaazaa hata iwapo mtoto alikuwa wa mwanamume huyu.

Masuala ya mtoto kando, nakubaliana vilivyo na maoni haya.

Ukweli ni kwamba mabinti wengi ambao huwa wamekubali kuwa sinia za pembeni hufahamu vyema kwamba dume husika lina mke.

Na wengi wao huwa wameridhika na makombo wanayopokea, mradi wananufaika kifedha.

Aidha mabinti hawa huwa wameridhika na nafasi ya pili maishani mwa dume hili.

Nafasi hii ya pili inamaanisha kwamba hauwezi lipigia simu, wala kulitumia arafa ya mapenzi hasa usiku wa manane.

Nakumbuka kisa cha binti mmoja aliyeridhika na nafasi ya pili ila akavunja masharti kwa kuanza kutuma meseji usiku wa manane. Kumbe alikuwa akimkera kaka ambaye sasa alimuona kama tishio kwa ndoa yake.

Siku moja kaka alimuita na kuvunja uhusiano huo bila hata kupepesa jicho.

Mbali na mawasiliano duni, pia, mikutano yenu ni ya kisiri ambapo mara nyingi atakubeba kwenye kiti cha nyuma cha gari. Kumbuka kwamba madirisha ya gari yake ni meusi hivyo hakuna anayekuona.

Iwapo utabahatika kuabiri kiti cha mbele kando yake, dirisha la mbele la abiria litasalia limefungwa hata jua likiwaka.

Hizi ni ishara za kudharauliwa.

Unakuta binti amevumilia kudhalilishwa huku kwote. Lakini mwanamume anapofariki, basi anadhani ni wakati wake kuwika.

Iwapo ulikuwa unataka kutambuliwa na kuheshimiwa, basi ungekataa kuwa katika uhusiano wa dharau na kumsaka mwandani wako.

Na kama ilikuwa lazima uwe katika uhusiano na mwanamume aliyeoa, basi haungekubali sarakasi hii ya kufichwa kiholela. Ungelisukuma dume hili likiwa hai likutambulishe hata ikiwa ni kama mke wa pili.