FATAKI: Nani kasema mwanamke hana haki ya kukata kiu ya mahaba?

FATAKI: Nani kasema mwanamke hana haki ya kukata kiu ya mahaba?

NA PAULINE ONGAJI

Siku chache zilizopita, rafiki yetu alitusimulia jinsi katika mojawapo ya ziara zake sehemu fulani nchini, alivyokumbana na kaka mmoja aliyemmaliza kiu yake ya mahaba.

“Tulikutana katika hoteli ambapo nilikuwa nimekodi chumba, naye pia alikuwa hapo kwa shughuli zake za kibiashara. Baada ya mazungumzo katika mkahawa wa hoteli hiyo, ashiki zilitupanda kisha tukaamua kwenda chumbani mwangu kumaliza haja,” akasema binti huyo.

Kulingana naye, alipokea mahaba ya kipekee, uhondo ambao hajashuhudia katika muda mrefu. “Na sikutaka chochote zaidi. Ilipofika asubuhi, tulioga, tukafuata staftahi, kisha kila mmoja akaenda njia zake hata bila kubadilishana nambari za simu,” akaongeza.

Burudani aliyopata binti huyo ilikuwa baada ya ukame wa zaidi ya mwaka mmoja, kwani katika kipindi hiki chote hajaonana na mchumbake anayefanya kazi ng’ambo.

Mazungumzo hayo yalinikumbusha dhana ambayo imekuwa ikiendeshwa kwa muda mrefu kwamba inapowadia katika masuala ya mahaba, mara nyingi mwanamume ndiye huwa mnufaishwa wa kitendo hicho.

Kwa upande mwingine, mwanamke amekuwa akitarajiwa kufaidika kutokana na shukrani hasa ya fedha kutoka kwa mwanamume.Nasema haya kwani katika jamii nyingi, tangu jadi, baada ya tendo la ndoa hasa la “haramu”, mwanamume huchukuliwa kuwa jogoo, huku mwanamke aliyemgawia kaka asali akionekana kuwa kahaba, kipusa asiye na msimamo thabiti kimaadili, au binti anayetaka kunufaika kutokana na chombo alichopachikiwa katikati mwa mapaja.

Ni dhana ambayo imekuwa ikiendeshwa kiasi kwamba wengi hudhani kwamba mwanamke hana hisia kufurahia tendo hili. Mabinti pia hufurahia mahaba na kuzima kiu yao, pasipo kutarajia chochote kutoka kwa mwanamume.

Pengine alikoenda kaka huyo alijipiga kifua na kujidai jinsi alivyofanikiwa kumtwanga binti huyu hata “bila kutoa jasho” wala senti mfukoni mwake kupunguzwa, na kusahau kwamba pia binti alikuwa na kiu na mahitaji yake.

Kumbuka kwamba kuna wanawake wasiotarajia chochote kutokana na raha ya mahaba. Hata kunao ambao wako tayari kulipia chumba na gharama zingine zinazotokana na shughuli hii.

Kwa hivyo suala la mahaba halipaswi kuchukuliwa kila mara kama taji la ushindi kwa mwanaume, na aibu kwa mwanamke.Pia jamii inapaswa kukoma kutumia suala la mahaba kama kigezo cha kupima kiwango cha uadilifu wa mwanamke.

You can share this post!

Aliacha kazi ya udaktari kufuga nguruwe na kukuza migomba

CHOCHEO: Mume si suti, ni ujasiri!