FATAKI: Ni upumbavu kuamini thamani ya mwanamke hushuka akizaa

FATAKI: Ni upumbavu kuamini thamani ya mwanamke hushuka akizaa

Na PAULINE ONGAJI

KUNA hii dhana potovu kwamba mwanamke akizaa au umri wake kuongezeka, basi thamani yake vile vile kiu ya madume hupungua.

Huenda dhana hii ya kuzaa imetokana na msemo maarufu katika baadhi ya jamii, unaolinganisha mwanamume kumtunga mwanamke mimba na kumvunja mguu, kumaanisha kwamba hawezi kuondoka zizini.

Imetumika kama kijisababu na baadhi ya wanaume wanaodhani kwamba wakishamzalisha mwanamke au kumpotezea wakati, basi hakuna mwanamume anaweza akatamani kumkaribia.

Hii inanikumbusha kisa cha binti mmoja aliyenisimulia jinsi mchumbake alivyobadilika baada ya kumzalisha mtoto wa pili.

Kulingana naye, kabla ya kujifungua mtoto wao wa kwanza, kaka alikuwa amemuahidi kwamba wangefanya harusi.

Hata hivyo pindi baada ya kujifungua, kaka akageuka bubu.

Ni lugha ambayo kaka huyo alirejea nayo binti huyu alipotishia kumuacha ambapo alimbembeleza tena kwa ahadi hizi za uwongo na kumtunga mimba ya pili na matokeo yakawa ni yale yale. Dume halizungumzii suala la ndoa tena.

“Siku hizi nikimuuliza ananiambia hana pesa wala muda wa ndoa na hakuna popote naweza enda kwani hakuna mwanamume anayeweza nioa na watoto wawili,” binti akamwaga ya moyoni.

Ni dhana ambayo imewapotosha wanaume wengi ambao wameishia kujuta baada ya kuwapoteza wachumba au wake wema.

Nakumbuka jamaa yangu mmoja aliyekuwa na mazoea ya kumtesa na kumsumbua mkewe eti kwa sababu alikuwa amemzalisha watoto watano.

Kulikuwa na tetesi kuwa dume hili lilileta vimada nyumbani na hata kulala nao chumbani mwao bila kujali.

Mara nyingi alikuwa akisema, “huyu hata nimfanyie nini hawezi ondoka. Ataenda wapi na watoto hawa wote?”

Ole wake kwani siku ya nyani kufa iliwadia ambapo alipokonywa mke na jirani yake bwanyenye aliyekuwa akimmezea mate mwanamke yule kwa muda mrefu.Huo ndio uhalisia wa maisha.

Kuzaa au umri hakulizuii dume fulani huko nje kudondokwa na mate linapomtazama mkeo.

Mwanamke anaweza kuwa ameolewa na hata kuzaa watoto 10, lakini bado kuna wale wanaovutiwa naye huko nje, na usipokuwa mwangalifu utapokonywa peupe!

You can share this post!

HUKU USWAHILINI: Biashara kwetu zina raha zake

Muturi aahidi kutumia wahitimu wasio na ajira katika vita...

T L