FATAKI: Raha jipe mwenyewe dada, siache vigezo vya jamii vikunyime starehe

FATAKI: Raha jipe mwenyewe dada, siache vigezo vya jamii vikunyime starehe

Na PAULINE ONGAJI

SIKU kadhaa zilizopita kulikuwa na mjadala ulioibuliwa na maoni ya kaka mmoja kuhusu binti fulani.

“Bibi huyo anakaribia umri wa miaka 50 na mavazi yake hayaakisi kamwe umri wake. Ukishafika orofa fulani maishani unapaswa kuachana na nguo za kubana, kwani mavazi haya yanakufanya uonekane mpumbavu,” akasema kwa kejeli.

Maoni haya yalinikera sana.

Kadhalika yalinikumbusha picha fulani kumhusu gwiji wa muziki wa Rock and Roll kutoka Amerika, Tina Turner.

Picha hiyo inalinganisha picha mbili za mwanamuziki huyu, moja akiwa katika umri wa miaka 47 na nyingine akiwa na miaka 74.

Kinyume na matarajio kwamba katika picha ya pili anapaswa kuwa amezeeka na dhaifu, bibiye anavutia hata zaidi uzeeni. Ni sawa na picha nyingine ya muigizaji Kenya Moore pia kutoka Amerika, ambaye umri na mwonekano wake unakinzana kabisa.

Nikimrejelea Tina Turner, licha ya umri wake ambao baadhi ya watu wanaweza utaja kuwa mkubwa, amedumisha mwili, msisimko na nguvu ambazo zaweza msababisha binti wa umri wa miaka 20 kujawa na wivu.

Mwanamke ambaye amedumu katika fani ya muziki kwa zaidi ya miongo mitano na kuandaa maelfu ya shoo, na ana mwonekano ambao utaacha mabinti wengi wachanga wakisakamwa na wivu.

Anawaibisha wale ambao wanadhani kwamba mwanamke akitimu miaka 30 na zaidi, basi usichana wake umekwisha na hivyo zamu yake ya kupendeza inaelekea kuisha.

Huenda kwa kweli amefanyiwa taratibu mbalimbali hapa na pale, lakini hauwezi afikia huo mwili, makalio hayo thabiti, hicho kiuno cha kuvutia na hiyo miguu ya kupindua vichwa njiani, kwa kufanyiwa upasuaji pekee; bibi huyo amejishughulikia vilivyo.

Hili ni funzo kwamba vigezo na vikwazo ambavyo jamii imeweka hasa dhidi ya mwanamke, havipaswi kukufungia raha yako licha ya umri kusonga.

Kama binti unapaswa kuelewa kuwa umri kamwe si kizingiti kuafikia lolote maishani.

Fanya mazoezi, kula vyema na ufurahie maisha pasipo kufikira jinsi jamii inavyokutarajia kuonekana ukitimu miaka fulani.

Tina Turner, Kenya Moore na wengine kama wao, ni funzo kwa hilo dume na wenzake wenye mawazo sawa na yake, vile vile kwa wanawake walioamua kupuuza mionekano yao kwa kisingizio cha umri.

You can share this post!

Mtihani mgumu kwa Arsenal ugenini Etihad

TAHARIRI: Spoti: Serikali iwazie miundomsingi zaidi