Pambo

FATAKI: Tumalize dhana na fikra potovu kabla ya kuamua kuwakosoa wale wanaojichubua ngozi

April 21st, 2024 2 min read

NA PAULINE ONGAJI

HIVI majuzi nilikuwa mtandaoni na kukumbana na video ya Bi Zozibini Tunzi, malkia wa urembo kutoka Afrika Kusini, aliyeshinda taji la urembo la Miss Universe mwaka wa 2019.

Ushindi wake uliibua mjadala mwaka huo kwani alikuwa mwanamke wa kwanza wa Kiafrika kushinda bila nywele za bandia.

Aidha, kilichoonekana kuchochea ushindi wake, ilikuwa ngozi yake nyeusi ambayo ilikuwa halisi.

Ushindi wake ulivutia mjadala mkuu mtandaoni huku wengi (hasa wanaume) wakionekana kuwahimiza mabinti wa Kiafrika kutoka kila pembe ya ulimwengu, kujivunia weusi wao badala ya kujichubua.

Nakumbuka wakati huo, mjadala huo uliibua maneno maarufu miongoni mwa watu weusi kwamba black is beautiful, msemo unaotumika kuwahimiza watu weusi kufurahia rangi ya ngozi yao.
Kupitia jukwaa hili watu weusi na hasa wanawake waliochibua ngozi zao ili kuwa weupe walikashifiwa na kurushiwa cheche za matusi.

Mimi pia ni mmoja wa wanaokashifu matumizi ya mafuta haya ya kuchibua ngozi kwani pia ni hatari kwa afya, lakini kabla ya kuwahukumu wenzetu wanaofanya hivyo, nani ashawahi jiuliza nini kinachowasukuma watu na hasa baadhi ya wanawake wa Kiafrika kutaka kuchubua ngozi zao?

Tunaishi katika jamii ambapo mwanamke mwenye asili ya kizungu au mweupe, ndiye anayesemekana kuwa mrembo.

Fikra hii potovu kadhalika imeendelezwa hasa na wanaume wa Kiafrika kupitia muziki wa kisasa ambapo asilimia kubwa ya nyimbo nyingi zinazoimbwa na hawa kaka zetu, kwa kiwango kikubwa zinawaonyesha mabinti wazungu au weupe zaidi kuwa warembo kuliko wenye ngozi nyeusi.

Swali langu ni vipi tutazidi kuyalaumu mataifa ya magharibi, vilevile vyombo vya kimataifa, ilhali katika jamii yetu ubaguzi dhidi ya wenye ngozi nyeusi umekita mizizi?

Ni mara ngapi umeskia misemo kama vile rangi ya thao, kumaanisha ngozi nyeupe na inayohusishwa na utajiri?

Hebu fikiria ni mabinti wangapi weusi wanaodunishwa na misemo ya aina hii, na kusalia na makovu maishani?

Ni wasichana hawa ndio watakuwa wa kwanza kutafuta suluhu ya kutaka kupendwa kama wenzao, hata ikiwabidi kuhatarisha afya zao ili kuwa weupe.

Hata sasa yameanza kuathiri madume wa Kiafrika. Siku hizi hata baadhi ya akina kaka zetu hasa kutoka Afrika ya kati na magharibi wanajichubua, pia kuonekana “watanashati”.

Kwa hivyo kabla ya jamii kuwahukumu hawa mabinti sharti dhana na fikra za utumwa zimalizwe.