Makala

Fatalaiza ya bei nafuu, kero la nzige msimu wa upanzi ukianza

March 29th, 2020 3 min read

Na CHARLES WASONGA

NI afueni kwa wakulima wa eneo la North Rift baada ya serikali kutangaza mipango ya kutoa mbolea wanapojiandaa kwa msimu wa upanzi.

Chini ya mpango huo serikali itanunua mbolea kutoka kwa watengenezaji. Kisha mbolea hii aina ya DAP itauzwa kwa wakulima kwa kupitia depo za Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) na maghala ya Shirika la Kitaifa la Wafanyabiashara (KNTC) kwa bei ya Sh2,300 kwa gunia moja la kilo 50.

Wafanyabiashara wa reja reja wamekuwa wakiwauzia wakulima mbolea hii ya kupanda kwa Sh3,200, bei ambayo wakulima wamelalamikia wakidai ni juu zaidi.

“Kuanzia msimu ujao wakulima watanunua mbole kutoka kwa maghala ya NCPB na KNTC kwa kutumia mfumo wa “e-Vouchers” ili kuwakinga dhidi ya gharama ya juu ya uzalishaji,” Waziri wa Kilimo Peter Munya akasema.

Alisema vocha hizo za kidijitali zitatolewa kupitia vyama vya ushirika vilivyosajiliwa ili kuwawezesha wakulima wadogo kufaidi kutokana na mpango huu.

“Mfumo huu umeanza kufanyiwa majaribio katika baadhi ya kaunti na lengo letu ni kuwafikia wakulima wenye mahitaji zaidi kupitia vyama vya ushirika vilivyosajiliwa,” Bw Munya akasema wiki jana walipokutana na wakulima kutoka eneo la North Rift mjini Eldoret.

Lakini wakulima waliiomba serikali kuzitekeleza kupitia Muafaka wa Maputo wa 2003, ambao Kenya ilitoa sahihi, na itenge angalau asilimia 10 ya bajeti ya kitaifa kwa sekta ya kilimo.

“Muafaka wa Maputo uliungwa mkono na Mkataba wa Malabo wa 2014 kuhusu malengo ya maendeleo endelevu na hivyo serikali inapasa kuutekeleza ili kupiga jeki sekta ya kilimo,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Muungano wa Wakulima Nchini (KFA) Kipkorir Arap Menjo.

Wakulima wa mahindi kutoka eneo hilo hata hivyo wamepata pigo kufuatia uvumazi wa nzige ambao huenda wakaathiri msimu huu wa upinzani.

Makundi ya nzige yamevamia sehemu kadha za kaunti za Trans Nzoia, Bungoma, Elgeyo Marakwet, Baringo, Pokot Magharibi na Turkana na kuharibi ekari kadhaa za mashamba ya mimea ya chakula na nyasi. Uvamizi huu ni tisho kuu kwa uzalishaji wa chakula na mali nyingine katika sehemu hizo.

Wakulima waliohojiwa walielezea hofi kwa nzige hao watakula mimea ya mahindi, wimbi, mtama na maharagwe wakati huu ambapo mvua imeanza kunyesha katika sehemu hizo.

“Nzige hao wamezaa mayai ambayo huenda yakaongolewa baada ya majuma machache yajayo na huenda wakala mimea yetu na kutupa hasara kubwa kwani tutalazimika kupanda tena,” akasema Mathew Kosgei mkulima kutoka eneo bunge la Moiben, kaunti ya Uasin Gishu ambako wadudu hao walionekana juzi.

“Nzige hao watarudisha nyuma mafanikio ambayo yaliandikishwa katika sekta ya kilimo kupitia upanzi kwa wakati ambapo wakulima wanatarajia kupata mavuno mazuri mwaka huu,” akaongeza Bw Kosgei.

Katika kaunti ya Trans Nzoia wakulima wa mahindi wanapanga kuchelewa kupanda baada ya makundi ya nzige kuonekana katika maeneo ya Matumbei, Kapretwa na Mankhele.

“Nzige walionekana katika kaunti hii na inashukiwa kuwa wametoka Uganda kupitia shamba la Shirika la Ustawishaji Kilimo (ADC) la Suam,” akasema Waziri wa Kilimo katika kaunti ya Trans Nzoia Mary Nzoma.

Alisema wamewashauri wananchi kuwa waangalifu na wapige ripoti endapo watawaona wadudu hao popote.

“Wao hula nyasi lakini huenda wakala mimea endapo hatua hazitachukuliwa haraka kuwaangamiza. Tumeanza mikakati ya kuwanyunyizia dawa,” akasema Bi Nzomo.

Katika kaunti za Uasin Gishu na Nandi maafisa wa idara za Kilimo walisema wameweka mikakati ya kukabiliana na wadudu hao waharibifu walioonekana katika kaunti jirani.

Waziri wa Kilimo katika Kaunti ya Nandi Dkt Kiplimo Lagat alisema wamewaita maafisa wao walioenda likizo ili wapige jeki juhudi za kupambana na nzige hao kote katika kaunti hiyo.

“Tumewaamuru maafisa wa kilimo wawe chonjo na wawasaidie wakulima katika kaunti ndogo za kaunti hii endapo nzige watavamia,” akasema.

Katika kaunti ya Elgeyo Marakwet nzige wamevamia maeneo la Soi Kusini, Tambach na Emsoo katika eneo bunge la Keiyo Kaskazini na kuibua hofu miongoni mwa wakulima.

“Nzige walitoka eneo la Chesongon kutoka kaunti ya Pokot Magharibi na wakatuvamia katika kijiji cha Liter. Walivamia nyanya na maembe kabla ya kuhamia maeneo ya Tiaty. Wakulima wameingiwa na hofu na wanaitaka serikali kuchukua hatua za kuangamiza wadudu hao,” akasema Bi Zephaniah Kiptoo mkaazi wa kijiji hicho.

Kulingana na Katibu wa Wizara ya Kilimo Prof Hamadi Boga, serikali hutumia Sh20,000 wa saa kunyunyizia nzige dawa kwa kutumia ndege.

“Nzige ni hatari kwa usalama wa chakula nchini na maisha ya wakulima kwani hula tani nyingi ya chakula ambacho kingeliwa na familia za eneo athirika,” akaeleza Prof Boga.

Wataalamu tuliowahoji walisema uvamizi wa nzige katika eneo la Kaskazini mwa Kenya unaweza kuchangia kushuka kwa uzalishaji wa mahindi kwa kiwango kikubwa.

“Hali itakuwa mbaya zaidi kwani mwaka jana kiwango cha mavuno ya mahindi kilishuka kwa magunia milioni 11, kutoka magunia milioni 44 mwaka wa 2018 hadi magunia milioni 33,” akasema Mathew Langat ambaye ni mtaalamu wa kilimo mjini Eldoret.

“Kwa kuwa nzige wamekula mimea mingine eneo hilo majuzi, kuna hofu kwamba huenda wakavamia mashamba ya mahindi na hivyo kuathiri uzalishaji wa chakula mwaka huu,” akaongeza.