Michezo

Fatuma Zarika aahidi kurejea nchini na taji lake la dunia

November 15th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Fatuma Zarika ameahidi kurejea nchini Kenya na taji lake la dunia la Baraza la Ndondi Duniani (WBC) atakapolimana na raia wa Mexico, Yamileth “Yeimi” Mercado katika uzani wa “Super Bantam” katika ukumbi wa Poliforo mjini Chihuahua mnamo Novemba 16, 2019.

Katika mahojiano na vyombo vya habari wakati wa shughuli ya kupimwa uzani na afya mnamo Novemba 14, Zarika, ambaye alibeba taji alipolima Yeimi mnamo Septemba 8 mwaka 2018 kwa wingi wa alama (99-91, 97-93, 94-96) jijini Nairobi, aliongeza kuwa anatarajia pigano kali.

“Nafurahia sana kufika nchini Mexico anakotoka Yamileth. Alikuja Nairobi kupigana nami na sasa nazuru kwake. Najua itakuwa mechi ngumu, lakini makonde yangu ndio yatakayozungumza siku ya pigano. Najua nitarudi nchini Kenya na taji langu,” alisema Zarika ambaye rekodi yake ni ushindi 30 (17 kwa njia ya KO), sare mbili na kupoteza mara 12.

Bondia huyo mwenye umri wa miaka 34 anakutana na Yeimi anayejivunia rekodi ya ushindi 12 (nne kwa njia ya KO) na kupoteza pigano moja.

Mercado ameapa hatapoteza pigano hilo nchini mwake.

“Pigano hili ndilo muhimu katika maisha yangu ya ubondia. Kuvua Zarika ubingwa nchini Mexico ni motisha kubwa na hiyo ndio sababu tulijandaa vyema kabisa. Niko tayari kutimiza lengo langu. Sitapoteza pigano hili. Ni heshima kubwa kupigania taji la dunia nyumbani. Nashukuru kila mtu aliyefanikisha pigano hili kuandaliwa nchini Mexico,” alisema bondia huyo mwenye umri wa miaka 21.

Zarika ataingia pigano hili la raundi 10 baada ya kushinda mapigano yake sita yaliyopita naye Yeimi ameshinda mapambano matano mfululizo na kupoteza moja kati ya sita yaliyopita.