FAUSTINE NGILA: Afrika isipojipigia debe Wikipedia itasahaulika

FAUSTINE NGILA: Afrika isipojipigia debe Wikipedia itasahaulika

Na FAUSTINE NGILA

HIVI, umewahi kujiuliza ni kwa nini watu mashuhuri katika siasa, michezo, burudani, elimu, sayansi na hata uanahabari humu nchini bado hawana wasifu katika tovuti ya Wikipedia?

Inashangaza kuwa mwanamuziki na mtunzi hodari kama Nikita Kering hana ukurasa wake katika Wikipedia, licha ya kuwika barani Afrika katika nyimbo zake zenye mvuto.

Na wale ambao utapata habari zao kwenye Wikipedia, taarifa hizo si kamilifu, zimejaa mapengo kadhaa na kukosa kuelezea kwa kina ufanisi waliopata kutokana na juhudi zao.

Hata baada ya wanahabari kuchapisha na kutangaza matukio ya kuvutia na kutia moyo katika magazeti, mitandao, redio na runinga kuhusu watu waliofanya makuu, tumekuwa wazembe wa kutambua umuhimu wa kutangaza talanta na maendeleo katika nchi yetu.

Ni majuzi tu ambapo ukurasa wa mshindi wa Tuzo ya Nobel mwendazake Prof Wangari Maathai ulihaririwa na kuchapishwa upya katika mtandao wa Wikipedia, lakini ukurasa wa mwigizaji hodari marehemu Charles Bukeko ‘Papa Shirandula’ umesalia kuwa na taarifa finyu licha ya juhudi zake katika kukuza vipaji vya uigizaji nchini.

Kenya imejaliwa kuwa na mwanasayansi wa kinuklia wa kwanza duniani wa rangi nyeusi Dkt Fridah Mokaya lakini taarifa halisi kumhusu hazijulikani kutokana na ukosefu wa Wakenya wazalendo ambao wanafaa kutumia taarifa za kweli na kina zilizochapishwa na wanahabari kuanzisha ukurasa kumhusu.

Majuzi nilihudhuria mkutano wa wahariri ulioandaliwa na wakuu wa mradi wa Afrocine ukishirikiana na Wakfu wa Wikimedia na Wikipedia ambapo niligundua sababu kuu ya ukosefu wa waandishi wa kurasa za Wakenya mashuhuri ni ukosefu wa uhamasisho hasa kutoka kwa serikali kuhusu haja ya kupigia debe Brandi Kenya.

Nchini Amerika, mtu yeyote anayefanya jambo la maana kwenye jamii, siasa au Sanaa hutambulika sana, wakiwemo watoto wenye vipaji vya kuvutia, na taarifa kuwahusu huandikwa kwa kina, kurasa zaidi ya kumi.

Ndio maana ndoto ya kila Mwafrika ni siku moja kusafiri nchini Amerika kujionea kwa macho mambo wanayosoma kwenye Wikipedia na kutazama kwenye filamu mbalimbali.Usishangae kung’amua kuwa kulingana na tafiti nyingi, Afrika imechangia chini ya asilimia moja pekee katika taarifa zote zilizochapishwa kwenye intaneti, zikiwemo picha, video, grafiki na matini!

Ni kweli kuwa teknolojia ya intaneti iliundwa na mataifa yaliyoendelea lakini haidhibitiwi na taifa lolote. Mataifa hayo yamejikaza kupakia matini kwenye intaneti mno, na ndio maana ukisaka neno ‘hand’ kwenye Google, ukienda kwenye picha, utapatana na mikono ya Wazungu tu.

Kwa kuwa sasa kila taifa barani Afrika lina intaneti, simu za kisasa na tarakilishi, ni wakati wa Waafrika wote watambue kuwa iwapo wananuia kusikika duniani, basi taarifa zao kwenye intaneti zinafaa kuongezeka.

Dunia itaendelea kupuuza Afrika tusipojipigia debe. Tupakie taarifa zilizothibitishwa kwenye Wikipedia, Google, YouTube, Vimeo, Facebook, Twitter, TikTok, Instagram, Snapchat, LinkedIn na katika wavuti za habari na makala ili angalau tuinue asilimia ya taarifa zetu kwenye intaneti hadi tano.

Utakuwa ni uzembe wa hali ya juu iwapo miaka kumi ijayo bado Afrika itakuwa ikitazamwa kama ‘bara jeusi’ na mabara mengine kwa kukosa kujitangaza kwa dunia kama bara lenye watu wa akili shupavu, wachapa kazi na waliostaarabika.

You can share this post!

Washukiwa 16 wakamatwa kwa kuitisha wakazi Mukuru pesa

LEONARD ONYANGO: Serikali itoe chakula cha msaada kwa...

F M