Makala

FAUSTINE NGILA: Shirika la Utafiti wa Angani limezembea mno, ligutuke

December 24th, 2020 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

Katika ukurasa wake wa Facebook, Shirika la Utafiti wa Angani la Kenya (KSA) lilichapisha habari hapo Desemba 8. Kwenye Twitter, liliweka posti Desemba 14.

Katika ulimwengu ambao mataifa yanayoendelea yanawapasha wananchi wake habari za angani kila uchao, inashangaza kwwamba Kenya – inayojizatiti kufuata nyayo za Afrika Kusini katika ulingo huu wa utafiti kuhusu anga ya dunia na sayari zingine – inatoa habari baada ya wiki kadha, tena kama vidokezo.

Nikivinjari kwenye Twitter, Shirika la Usimamizi na Utafiti wa Angani la Amerika (NASA) huchapisha habari mpya mara nne kila siku, jambo ambalo limevutia wafuasi milioni 46 na wengine milioni 25 katika ukurasa wake wa Facebook.

Licha ya kutengewa mamilioni ya pesa katika bajeti, KSA inaonekana kulemewa na jukumu ililotwikwa na Wakenya. Kutokana na mtindo wake wa kuwanyima wananchi habari mitandaoni, shirika hilo lina wafuasi wachache mno – 600 Twitter na 64 Fabebook!

Hii inamaanisha kuwa halifanyi kazi yake inavyostahili; halichapishi ripoti za tafiti mbalimbali ulimwenguni kwa manufaa ya wananchi kung’amua maendeleo ya sasa; halilinganishi teknolojia za wavumbuzi mbalimbali; na huenda ndio maana halina chochote cha kuwaambia wananchi.Wakenya wangependa kuarifiwa kuhusu jitihada za taifa lao katika mpango mzima wa kutafiti kuhusu anga ya sayari.

Hususan ni lini itaweza kutuma chombo angani kukusanya data kama mataifa yanayoendelea.Ingawa mwaka huu KSA ilitoa Sh5 milioni kufadhili utafiti wa hali ya hewa kwa vyuo vikuu vya Eldoret, Dedan Kimathi na Taifa Taveta; kama taifa ambalo limejaliwa vipaji vya teknolojia, vizingiti katika kutoa habari za utafiti havifai kushuhudiwa.

Kenya, inayojipiga kifua kama mbabe wa utafiti wa kiteknolojia barani Afrika, inafaa kuchangia pakubwa katika utoaji wa habari muhimu kuhusu anga ya bara hili.

Utafiti unaonyesha kuwa kutokana na ukosefu wa data kuhusu mawimbi katika sehemu mbalimbali za njia za ndege angani, kampuni za ndege hupoteza Sh5 trillioni kila mwaka kwa sababu ya kucheleweshwa kwa safari za ndege, ambazo huishia kuelekezwa katika njia mbadala.

Sekta ya utalii inategemea mno utafiti huu kwani husaidia watalii kuamua iwapo watasafiri mataifa fulani. Kuvurugwa kwa mawimbi yanayotumika kufanikisha mawasiliano ya rubani anayeendesha ndege na viwanja vya ndege, husababisha kuchelewa kwa abiria.

Zaidi, kujua ni wapi mawimbi hayo yatasababisha mtingiko wa ndege angani, ndizo habari muhimu sana katika sekta ya usafiri wa ndege.

Inachofanya Kenya ni kutegemea watafiti wa mataifa ya ng’ambo kama Amerika, China na Urusi, bila kujali kuwa anga zote ni tofauti kutokana na mvuto wa jua kwa dunia.

Tunaishi katika dunia inayobadilika kwa kasi, ukizingatia kuwa Amerika sasa ishaanza mpango wa kupeleka watalii angani ili wakaishi katika sayari nyinginezo, kutokana na machafuko ya hewa na mabadiliko ya tabia nchi kila mwaka.

Hayo tumeyajua kutokana na habari zinazochapishwa na NASA. Je, KSA isipotuarifu mitandaoni kuhusu mipango yake tutaijuaje?

[email protected]