HabariKimataifa

FBI wachunguza aliyemtumia Trump sumu kwa bahasha

October 3rd, 2018 2 min read

Na AFP

WASHINGTON, AMERIKA

IDARA ya Upelelezi ya Amerika (FBI) inafanya uchunguzi kubainisha aliyemtumia Rais Donald Trump na maafisa wake wakuu wa ulinzi barua iliyokuwa na sumu kali inayoweza kusababisha maafa kwa dakika chache.

Maafisa serikalini jana walisema barua inayoshukiwa kuwa na sumu ya ‘raicin’ ilipatikana katika Makao Makuu ya Ulinzi (Pentagon) ambayo ndiyo hupokea barua zote za rais.

Kitengo cha ulinzi wa maafisa wakuu serikalini, almaarufu kama Secret Service, kilisema barua hiyo ilipokewa Jumatatu na siku hiyo hiyo kuna vifurushi viwili ambavyo vilizuiliwa katika kituo cha kukagua barua za Ikulu.

‘Bahasha hiyo haikufika katika White House, wala hata kuingia mlangoni mwa Ikulu. Tunaweza kuthibitisha kwamba tunashirikiana na idara zingine za usalama kuchunguza suala hili kikamilifu,’ kitengo hicho kikasema kwenye taarifa.

Msemaji wa Pentagon, Chris Sherwood, alisema maafisa walipokuwa wakikagua barua zilizopokewa ‘walitambua kulikuwa na vifurushi ambavyo vilitiliwa shaka,’ akasema ‘ilishukiwa ni sumu ya ricin’.

Alisisitiza kwamba maafisa walikuwa wanasubiri thibitisho kwamba sumu hiyo ndiyo ilikuwa kwenye bahasha, na polisi wa Pentagon wakawasilisha suala hilo kwa FBI ili lichunguzwe zaidi.

Afisa katika idara ya ulinzi alisema barua zingine zilikuwa zimetumwa kwa Waziri wa Ulinzi Jim Mattis na Mkuu wa Jeshi la Wanamaji, John Richardson.

Ingawa kitengo cha kupokea barua za ikulu kiko katika Pentagon, huwa kimetengewa sehemu yake kando na jengo hilo la makao makuu ya ulinzi.

Wafanyakazi hapo huvaa mavazi maalumu meupe ya kuwalinda kutokana na athari yoyote ya sumu,na hukagua kila barua inayoshukiwa kuwa na sumu hiyo ya ricin ambayo imekuwa ikitumiwa sana na magaidi.

Ricin ni sumu kali ambayo inaweza kusababisha kifo ikiwa mtu ataimeza, kuituta au kudungwa nayo kupitia kwa sindano. Ukali wake ni mara 6,000 ya sumu ya cyanide ambayo ni nyingine inayotambulika kwa ukali wake, na haina dawa ya kupunguza makali yake.

Inapoingia mwilini, mwathiriwa huanza kutapika, kuvuja damu ndani ya mwili na kupata matatizo ya kupumua kisha kifariki kutokana na kupooza kwa viungo muhimu vya mwili hasa vinavyosambaza damu.

‘Maafisa maalumu wa FBI walichukua bahasha mbili ambazo zilikuwa zimekaguliwa katika kitengo cha kupokea barua Pentagon. Bahasha hizo sasa zinafanyiwa uchunguzi zaidi,’ FBI ikasema kwenye taarifa.

Msemaji wa Idara ya Ulinzi, Kanali Rob Manning, alisema barua zote zilizopokea Jumatatu ‘zimehifadhiwa katika sehemu maalumu iliyotengwa’ na hivyo basi hakuna hatari yoyote kwa wafanyakazi wa Pentagon.

Awali watu wawili walilazwa hospitalini Houston, Texas, baada ya kuathiriwa na sumu iliyokuwa kwenye barua zilizotumwa kwa Seneta Ted Cruz, kwa mujibu wa mashirika ya habari.

-Imekusanywa na Valentine Obara