FC Barcelona katika mizani ya Alaves La Liga ikimsubiri Xavi

FC Barcelona katika mizani ya Alaves La Liga ikimsubiri Xavi

BARCELONA, Uhispania

Na MASHIRIKA

FC Barcelona itatumai kuanza maisha bila kocha Ronald Koeman kwa kishindo itakapoalika Alaves katika mchuano wa Ligi Kuu ya La Liga ugani Camp Nou.

Miamba hao wa Uhispania walitema Mholanzi Koeman mnamo Oktoba 27 baada ya msururu wa matokeo duni na wanaendelea kuhusishwa na kocha Xavi Hernandez wa Al Sadd, Qatar. Koeman alitimuliwa baada ya Barca kuambulia ushindi mara tatu pekee katika mechi 10 zilizopita katika mashindano yote.

Vyombo vya habari nchini Uhispania vilidai jana kuwa Xavi yuko pua na mdomo kurithi nafasi ya Koeman ambayo kwa sasa inashikiliwa kwa muda na kocha wa timu ya daraja la pili Sergi Barjuan.

Vyombo hivyo vilidai kuwa Xavi atasafiri hadi Barcelona kujiunga na timu hiyo mnamo Novemba 3.Katika mechi ya leo, nambari tisa Barca itajibwaga uwanjani bila pointi katika mechi mbili zilizopita baada ya kulemewa na mahasimu wao wa tangu jadi Real Madrid 2-1 na Rayo Vallecano 1-0.

Itakutana na Alaves ambayo imefufuka. Baada ya kupepetwa na Athletic Bilbao na Real Betis 1-0 na Osasuna 2-1, Alaves ilijitoa katika mduara wa kushushwa ngazi kwa kuadhibu Cadiz 2-0 na Elche 1-0. Barca imepoteza mara moja pekee ligini ugani Camp Nou msimu huu, kutoka sare mara moja na kushinda nne kwa hivyo Alaves iliyopata ushindi uwanjani humu mara ya mwisho Septemba 2016, bado ina kibarua kigumu.

Mshambuliaji matata wa Uholanzi Memphis Depay na raia wa Argentina Sergio Aguero watategemewa wakati huu ambapo Barcelona inakosa nyota saba wanaouguza majeraha wakiwemo Ansu Fati na Pedri. Joselu ndiye tegemeo la Alaves.

Leo pia itakuwa zamu ya Elche kugaragazana dhidi ya viongozi wa ligi Real Madrid, huku Sevilla ikilimana na Osasuna nayo Valencia ikikabana koo na Villarreal.

You can share this post!

Mtanange babkubwa

Macho yote kwa Shujaa,Morans Safari 7s ikianza

T L