FC Porto yaangusha miamba Juventus kwenye soka ya UEFA licha ya Taremi kuonyeshwa kadi nyekundu

FC Porto yaangusha miamba Juventus kwenye soka ya UEFA licha ya Taremi kuonyeshwa kadi nyekundu

Na MASHIRIKA

BAO la dakika ya 115 kutoka kwa Sergio Oliveira liliwezesha FC Porto kuwaduwaza Juventus katika mechi ya marudiano ya hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Machi 9, 2021.

Frikiki ya Oliveira kutoka nje ya hatua ya 18 ilipita katikati ya miguu ya Cristiano Ronaldo na kujaa kimiani mwa Juventus walioaga kampeni za UEFA msimu huu kwa jumla ya mabao 4-4.

Porto FC waliingia katika mechi hiyo wakijivunia ushindi wa 2-1 katika mkondo wa kwanza uliosakatwa mnao Februari 17, 2021 jijini Lisbon. Miamba hao wa soka ya Ureno walijikatia tiketi ya kusonga mbele kwa kanuni ya wingi wa mabao ya ugenini licha ya kusalia na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya fowadi Mehdi Taremi kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 54.

Oliveira aliwaweka Porto uongozini kupitia penalti ya dakika ya 19 baada ya Merih Demiral kumchezea Taremi visivyo ndani ya kijisanduku cha Juventus. Hata hivyo, Federico Chiesa alisawazishia waajiri wake katika dakika ya 49 kabla ya kuweka kikosi hicho cha kocha Andrea Pirlo kifua mbele kunako dakika ya 63. Bao la pili la Chiesa lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Juan Cuadrado.

Ilitarajiwa kwamba Juventus wangechuma nafuu kutokana na uchache wa wanasoka wa Porto uwanjani na kuzamisha chombo cha wageni wao kirahisi baada ya Taremi kufurushwa ugani dakika tisa pekee baada ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa kipindi cha pili kupulizwa.

Hata hivyo, wachezaji wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) walipoteza nafasi nyingi za wazi walizozipata kupitia kwa Ronaldo, Alvaro Morata na Chiesa. Juventus kwa sasa wamebanduliwa kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA kwa kanuni ya wingi wa mabao ya ugenini kwa msimu wa pili mfululizo.

Bao la pili lililofungwa na Oliveira dhidi ya Juventus mnamo Jumanne usiku lilitosha kuwarejeshea mashabiki wa Porto kumbukumbu za mwaka wa 2004. Wakati huo, kiungo Costinha Francisco Costa alifunga frikiki ya dakika ya mwisho dhidi ya Manchester United na kusaidia waajiri wake Porto kufuzu kwa robo-fainali za UEFA.

Ufanisi huo ulisaidia Porto kupata motisha kubwa iliyowawezesha kunyanyua ufalme wa kivumbi hicho msimu huo.

Miaka 17 baadaye, historia hiyo ilionekana kujirudia baada ya frikiki ya chini kwa chini iliyochanjwa na Oliveira kupita katikati ya miguu ya Ronaldo na kumwacha hoi kipa Wojciech Szczesny langoni mwa Juventus.

Kubanduliwa kwa Juventus kwenye UEFA msimu huu sasa kunamweka kocha Pirlo katika presha zaidi ikizingatiwa kwamba kikosi chake kinashikilia pia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Serie A huku pengo la alama 10 likiwatenganisha na viongozi Inter Milan.

Maswali mengi sasa yanatarajiwa kuibuliwa na mashabiki wa Juventus kuhusu kiini cha kuteuliwa kwa Pirlo aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Maurizio Sarri mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20 licha ya kiungo huyo mshindi wa Kombe la Dunia kutojivunia tajriba yoyote katika ulingo wa ukufunzi.

Ingawa Juventus wamefuzu kwa fainali ya Coppa Italia msimu huu, wamekuwa wakisuasua kwenye kampeni za Serie A licha ya kutawazwa mabingwa wa kivumbi hicho kwa mfululizo wa misimu tisa iliyopita.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Nkana FC anayochezea Mkenya Abuya yaendea muujiza dhidi ya...

Afisa wa GSU aangamiza wenzake wawili kwa risasi na...