Michezo

Fearless yasema ubingwa wa KYSD ni wao msimu huu

July 21st, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Fearless FC ni miongoni mwa vikosi vinavyopania kujituma kiume kwenye migarazano ya kufukuzia taji la Ligi ya KYSD kwa wavulana wasiozidi umri wa miaka 14 msimu huu wa 2019/2019.

Kikosi hiki kinasadiki kwamba msimu huu kimejipanga azma kuu ikiwa kubeba ubingwa huo baada ya kumaliza nafasi ya nne mara mbili mfululizo.

Kocha wake, Jonah Makau anasema “Ingawa kampeni za msimu huu zinapigiwa chapuo kushuhudia upinzani mkali ninaamini chipukizi wapya ambao tumesajili kwa ajili ya kipute hicho watachochea wenzao kufanya kweli.”

Kocha huyo anasema analenga kutumia huduma za sajili hao wapya maana wapinzani wao kamwe hawafahamu mchezo wao.

”Msimu huu hatuna la ziada mbali kwa mara ya kwanza tunataka kutuzwa mabingwa wa kinyangányiro cha KYSD,” nahodha wake, Immanuel Erkanes anasema na kuongeza kuwa licha ya azimio hilo wanafahamu kampeni za msimu huu hazitakuwa rahisi maana vikosi vyote vimeonekana vimejipanga kutifua kivumbi cha kufa mtu.

Fearless FC imekuwa ikishiriki ngarambe hiyo tangu mwaka 2012 ambapo licha ya kutoshinda taji hilo inajivunia kunoa talanta za chipukizi wengi tu wavulana na wasichana pia kuwapa mwelekeo mwafaka kimaisha. Fearless FC inashirikisha timu za viwango tofauti kwa wavulana na wasichana.

Inapatikana mtaani Shaurimoyo Kamukunji, Nairobi na huendesha masuala ya mchezo wa soka chini ya shirika la YMCA ambapo chipukizi kadhaa wamefanikiwa kupata ufadhili wa elimu yao katika Shule za Msingi.

Chipukizi wawili (U13), Jamaine Khamati na Rodney Okinyi bila kusahau mmoja (U15), Faiz Ouma kutoka Fearless FC wamebahatika kujiunga na kituo cha Acakoro ambacho bosi wake ni Stanley Okumbi aliyewahi kunoa timu ya taifa ya Harambee Stars.

Pia wapo wengine wamepata ufadhili wa masomo baada ya kuonyesha mchezo mzuri ambao ni:Ferruz Oyonde, Ruweida Wambui, Amina Mwanapwani na Jeffy Cyprian.

Pia imefanikiwa kutoa wachezaji kadhaa ndani ya miaka mitatu sasa ambao hujiunga na wenzao kupitia kituo cha MYSA kushiriki fainali za Norway Cup nchini humo.

Kwa kitengo cha wasichana wasiozidi umri wa miaka 13 imeshiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati tangu mwaka 2015 na kufaulu kumaliza ya pili mara mbili (mwaka 2017 na 2018).

Kwenye ngarambe ya mwaka huu Fearless FC ilishirikisha timu mbili za wasiozidi umri wa miaka 16, wavulana na wasichana ambapo kila moja ilimaliza nne bora. Kocha huyo anadokeza kuwa katika Kaunti ya Nairobi wameshiriki mashindano mengi tu ambapo mara nyingi humaliza kati ya tano bora.

Wavulana wa Fearless FC wanaoshiriki Ligi ya KYSD wanajumuisha: Fabian Otsola, Michael Sunguti, Kelvin Maina, Kennedy Mwendwa, Immanuel Erkanes, Jamaine Khamati, Kevin Muthoka, Onesmus Muthoi, Spenser Mukhaba na Emmanuel Maina.