HabariSiasa

FEDHA: Wizara ya nuksi

July 24th, 2019 2 min read

VALENTINE OBARA Na BENSON MATHEKA

MASAIBU yanayomkumba Waziri wa Fedha, Henry Rotich yameongeza jina lake kwenye orodha ya walioandamwa na mikosi ya madai ya ufisadi na usimamizi mbaya wa fedha katika wizara hiyo.

Kulingana na Rais Uhuru Kenyatta alipohutubia Bunge mnamo Aprili, Bw Rotich sasa ameng’atuka ofisini.

Bw Rotich ameshikilia wizara hiyo tangu Jubilee ilipotwaa uongozi wa nchi mnamo 2013, na atakumbukwa kwa kuacha Kenya katika utumwa wa madeni, hali ngumu ya kiuchumi na ushuru wa juu.

Baadhi ya mawaziri waliomtangulia katika wizara hiyo walijipata wakilazimika kujiuzulu ama wakiandamwa na kashfa hata baada ya kuondoka ofisini.

Mnamo Julai 2008, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Amos Kimunya alijiuzulu siku chache baada ya kuapa kwamba heri afe kuliko kujiuzulu kwa madai ya ufisadi.

Mbunge huyo wa Kipipiri alikuwa amehusishwa kwenye sakata ya uuzaji wa hoteli ya Grand Regency jijini Nairobi ambayo ilikuwa inamilikiwa na serikali.

Ilisemekana ufisadi uliofanywa katika uuzaji huo kwa wawekezaji wa Libya ulipelekea hoteli hiyo, ambayo sasa inafahamika kama Laico Regency, kuuzwa kwa bei ya chini kuliko thamani yake halisi.

Mnamo 2009, akiwa Waziri wa Fedha, Rais Uhuru Kenyatta alilazimika kufika mbele ya kamati za bunge zilizosimamia masuala ya fedha na bajeti kueleza kuhusu jinsi Sh9.2 bilioni zilivyojumuishwa kwenye bajeti ya ziada kwa njia isiyoeleweka.

Lakini akijitetea, Rais Kenyatta alidai fedha hizo zilijumuishwa kwenye bajeti kutokana na ‘hitilafu ya kompyuta’.

Ni wakati wa usimamizi wake katika wizara hiyo ambapo pia serikali iliagiza magari aina ya Volkswagen Passat ikidai yatasaidia kupunguza gharama ya mafuta kwa usafiri wa watumishi wa umma.

Lakini magari hayo hayakutumiwa ipasavyo kwani hadi sasa watumishi hutumia magari makubwa yanayonyonya mafuta. Alilaumiwa kwa kuharibu fedha za umma kwa ununuzi wa magari hayo.

Mnamo 2003, marehemu David Mwiraria aliteuliwa waziri wa kwanza wa fedha baada ya chama cha Kanu kuondolewa mamlakani.

Hata hivyo, chini ya usimamizi wake, wizara hiyo ilikumbwa na sakata ya Anglo Leasing ambapo Kenya ilipoteza zaidi ya Sh60 bilioni kupitia miradi feki ya kununua bidhaa zikiwemo za kijeshi.

Bw Mwiraria alijiuzulu 2006 baada ya kuhusishwa na sakata hiyo.

Mnamo 2016 iliamuliwa ashtakiwe kwa mchango wake katika sakata hiyo lakini akaaga dunia kabla ya kesi kuendelea.

Kashfa kuu ya kwanza ambayo iliandama mawaziri wawili waliohudumu katika wizara hiyo ilikuwa ya Goldenberg ambapo serikali ilipoteza zaidi ya Sh5.8 bilioni kupitia fedha ilizolipa mfanyabiashara Kamlesh Pattni kwa biashara feki ya dhahabu.

Kashfa hiyo ilianza miaka ya tisini wizara ilipokuwa ikisimamiwa na marehemu Prof George Saitoti na ilikuwa sababu yake kuhamishwa kutoka wizara hiyo mnamo 1993.

Mnamo 2006, ripoti ya uchunguzi uliofanywa na tume iliyosimamiwa na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Samuel Bosire ilipendekeza kuwa Prof Saitoti ashtakiwe.

Mnamo Februari 13, 2006, Prof Saitoti alijizulu wakati huo akiwa Waziri wa Elimu.

Hata hivyo hakushtakiwa na baadaye akafika kortini na kupata agizo la jina lake kuondolewa kutoka ripoti hiyo.

Mrithi wake katika wizara hiyo alikuwa Musalia Mudavadi ambaye kwa wakati huu ni kiongozi wa chama cha Amani National Congress.

Bw Mudavadi alisimamia wizara hiyo kwa miaka minne wakati ambao uchumi wa Kenya ulivurugika kuelekea uchaguzi mkuu wa 1997.

Ripoti ya tume ya Jaji Bosire pia ilipendekeza Bw Mudavadi kuitwa kueleza ilichotaja kama malipo yasiyokuwa ya kikatiba.