Habari MsetoSiasa

Fedha za umma zilizofujwa zirejeshwe upesi – Sapit

August 7th, 2018 2 min read

Na GERALD BWISA

SERIKALI imeombwa kushinikiza kurejeshwa kwa pesa zilizoibwa katika ufisadi huku juhudi zikiimarishwa kupambana na ufujaji wa pesa za umma.

Akizungumza na wanahabari Kitale Jumapili, Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana la Kenya, Jackson ole Sapit, alimwambia Rais Uhuru Kenyatta asilegeze kamba katika juhudi hizo.

Alisema inafaa mapambano dhidi ya ufisadi yaendelee hadi wakati pesa zote za umma na rasilimali zilizopotea zirudishwe na kutumiwa kwa manufaa ya wananchi.

“Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi na Idara ya Mashtaka ya Umma zimepiga hatua kubwa kwa kufikisha mahakamani wale wanaojihusisha katika ufisadi lakini haifai yaishie hapo. Kama kuna pesa zozote zilizopotea katika ufisadi inafaa zirejeshwe,” akasema.

Bw Sapit alisema kuna taasisi kama vile hospitali za umma ambazo zina uhaba wa mahitaji muhimu ilhali watu binafsi wanafuja pesa za umma.

“Tuna uhaba wa dawa hospitalini, pesa zinazofujwa zinafaa zirejeshwe ili zitumiwe kununua dawa hospitalini na pia kutumiwa kwa ujenzi wa miundomsingi kwa manufaa ya wananchi,” akasema.

Alitoa wito pia kwa bunge la taifa, hasa kamati inayochunguza sakata ya sukari kuhakikisha ripoti zinazotolewa zimezingatia ukweli uliopo.

Aliwataka wabunge wajiepushe kushawishiwa ili wafiche uweli bali waseme yote waliyobainisha kwenye uchunguzi wao.

Askofu huyo mkuu aliomba pia viongozi nchini wawe na malengo yatakayodumisha utulivu nchini hata wakati watakapoondoka mamlakani.

Alisema viongozi watakutana kufanya mashauriano kuhusu jinsi ya kuzuia changamoto zinazoweza kuweka vikwazo kwa utekelezaji wa malengo muhimu kwa taifa. Wakati huo huo, aliyekuwa Waziri wa Wanyamapori na Misitu, Dkt Noah Wekesa, aliunga mkono juhudi za rais kupambana na ufisadi.

Dkt Wekesa alisema ufisadi umeathiri maendeleo ya nchi. Alitoa wito kwa viongozi wa makanisa kuongoza Wakristo ili watekeleze majukumu yao ya kuchangia katika kupambana na ufisadi na kuhakikisha kuna mafanikio katika juhudi hizo.

“Rais ana ajenda nne anazolenga kufanikisha. Kwa mtazamo wangu akiendelea kupambana na ufisadi kwa moyo wake wote, hilo pekee litapewa umuhimu kuliko ajenda hizo nne kwa kuwa ufisadi umeelekeza nchi yetu pabaya,” akasema.