HabariSiasa

Fedha za wanasiasa mnazotumia kujenga makanisa ni chafu, Keter aonya

June 21st, 2018 2 min read

Na LEONARD ONYANGO
MBUNGE wa Nandi Hills Alfred Keter sasa ametaka viongozi wa kidini kukoma kujenga makanisa kwa kutumia pesa ‘chafu’ kutoka kwa wanasiasa.

Kulingana na Bw Keter wanasiasa wanaojihusisha na biashara ya sukari ya magendo inayodaiwa kuwa na sumu, ndio wanaotoa michango makanisani kila wikendi bila kuishiwa na fedha.

“Ukiona mwanasiasa anaongoza mikutano zaidi ya minne ya harambee  kwa siku na kila harambee anatoa fedha zisizopungua Sh2 milioni, huyo mwanasiasa anatoa wapi fedha hizo?” akauliza Bw Keter katika mahojiano na runinga ya NTV, Alhamisi asubuhi.

“Napenda kuwakumbusha viongozi wa kidini kwamba fedha mnazotumia kujenga makanisa ni chafu. Inasikitisha kuwa mnajenga makanisa matakatifu kwa kutumia fedha chafu,” akasema Bw Keter.

Mbunge huyo aliwataka viongozi wa kidini kuwahoji wanasiasa hao wanapotoa fedha ili kuthibitisha ikiwa pesa zinazotolewa katika michango zilipatikana kwa njia halali auni za wizi.

Bw Keter alidai kuwa maafisa wafisadi serikalini wanaiba Sh2 bilioni kila wikendi ambazo wanatumia kutoa katika harambee

“Kila mwaka Sh400 bilioni hupotelea katika mifuko ya wafisadi. Ikiwa wezi hao watapumzika kuiba siku ya Jumamosi na Jumapili, kila Wikendi Kenya itaokoa Sh2 bilioni. Kwa mwaka tutaokoa Sh96 bilioni,” akasema Bw Keter.

Mbunge huyo machachari kutoka Bonde la Ufa amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kutimua mawaziri husika walioshindwa kuzuia uingizaji wa bidhaa ya magendo nchini.

“Rais Kenyatta asilegeze kamba kuhusiana na vita dhidi ya ufisadi na uingizaji wa sukari ya magendo nchini. Kadhalika, namsihi rais kuwaachisha kazi baadhi ya mawaziri walioshindwa kuzuia uingizwaji wa bidhaa ghushi nchini,” akasema.

Bw Keter pia anataka maafisa wanaosimamia Shirika la Kuhakiki Ubora wa Bidhaa (Kebs), Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) na idara nyinginezo watimuliwe kwa kuzembea kutekeleza majukumu yao huku sukari ya magendo ikiingizwa nchini.

“Ili kuzuia siasa inayoendelea kuhusiana ikiwa sukari hiyo ya magendo ina sumu au la, waziri wa Usalama Fred Matiang’i ajitokeze aweke wazi ripoti kuhusiana na vipimo vilivyofanywa na kubaini kuwa sukari hiyo imechanganywa na madini ya mekyuri au la,” akasema Bw Keter.

Madai kuwa sukari ya magendo inayoendelea kunaswa katika maeneo mbalimbali imechanganywa na mekyuri, yaliyotolewa na Dkt Matiang’i, yamepuuziliwa mbali na mwenzake wa Viwanda Adan Mohamed na kuwaacha Wakenya katika njiapanda.

Mbunge wa Nandi alidai kuwa wafanyabiashara na wanasiasa wanaohusika na biashara ya sukari ya magendo wanawekeza fedha zao katika mataifa ya kigeni kama vile Dubai, Afrika Kusini, Zambia, Botswana kati ya mengineyo kwa kuhofiwa kukamatwa.