Felly Mulumba kuisakatia Bandari wikendi

Felly Mulumba kuisakatia Bandari wikendi

ABDULRAHMAN SHERIFF, MOMBASA

ALIYEKUWA mchezaji wa FC Platinum ya Zimbabwe, Felly Mulumba ni miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha timu ya Bandari FC kilichoondoka Mombasa Jumanne kuelekea Nairobi ambako inatarajia kupambana na Kariobangi Sharks FC siku ya Jumamosi.

Meneja wa Bandari FC Albert Ogari alisema timu yake iliondoka ikiwa na Mulumba ambaye alirudi kutoka Zimbabwe na kusaini timu yake ya zamani na atakuwako kwenye mechi ya Ligi Kuu ya FKF dhidi ya Sharks.

“Nathibitisha kuwa sentahafu wetu wa zamani Mulumba amerudi na yuko katika kikosi cha timu kilichoondoka kuelekea Nairobi na nina matumaini makubwa atacheza mechi ya Jumamosi,” akasema Ogari.

Meneja huyo pia alisema straika wao William Wadri aliyemaliza kifungo cha mechi mbili baada ya kupewa kadi nyekundu, yuko katika kikosi hicho kitakachokabiliana na Sharks na ana matarajio atacheza.

Ogari amesema wanakwenda jijini kujitahidi kupata pointi zote tatu ambazo zitawapandisha kwenye ngazi ya ligi hiyo inayozidi kuwa ya patashika kila timu ikipigania kuwa katika nafasi nzuri ama kushinda.

Hata hivyio, timu hiyo iliondoka bila ya wanasoka wawili, winga Shaaban Kenga ambaye angali anapata matibabu ya kuvunjika mguu na golikipa Michael Wanyika ambaye anaendelea kujiuguza maumivu ya goti.

Timu ya Bandari inakwenda Nairobi ikiwa na machungu ya kushindwa mabao 3-1 na Gor Mahia kwenye mechi iliyofanyika Mbaraki Sports Club, Jumapili iliyopita ambapo kocha Andre Cassa Mbungo alidai makosa makubwa yalikuwa katika safu ya ushambuliaji.

Mbungo alisema atafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanasoka wake wanatumia nafasi wanazopata hasa zile za mapema ili kuweza kuvunja nguvu wapinzani wao. “Nina imani kubwa kama tutapata kuzitumia nafasi za mapema, tutaweza kushinda mechi nyingi,” akasema kocha huyo.

You can share this post!

Siaya kaunti ya kwanza kupitisha BBI

Waigizaji wa Ukombozi Film wanavyonoa vipaji vya watoto...