Michezo

FEMENINO: Real Madrid wazindua kikosi chao cha soka ya wanawake

July 2nd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

REAL Madrid wamezindua kikosi chao cha soka ya wanawake, hatua ambayo imepongezwa pakubwa na mashabiki.

Usimamizi wa Real almaarufu Los Blancos, umethibitisha kukamilisha ununuzi wa kikosi cha Tacon kwa Sh38 milioni na kujitwalia umiliki. Klabu hiyo kwa sasa itajulikana kama Real Madrid Femenino.

Katika taarifa yao, Real wamesema wamekuwa na kiu ya kuchangia vilivyo maendeleo ya soka ya wanawake ndani na nje ya Uhispania.

“Wakati mwafaka wa kujijengea kikosi cha wanawake ambacho kitajivuniwa na kitastahiwa na wengi kwa kiwango sawa na kile cha wanaume umewadia. Tunawastahi sana vipusa wetu na kuzinduliwa kwa kikosi hiki ni hatua kubwa katika kuchangia maendeleo yao kitaaluma,” akasema Rais wa Real Madrid, Florentino Perez.

Real ilikuwa miongoni mwa vikosi vya haiba kubwa zaidi katika soka ya bara Ulaya kukosa timu ya wanawake.

Fowadi Ada Hegerberg wa Olympique Lyon amesema kuundwa na hatimaye kuzinduliwa kwa Real Madrid Femenino ni hatua kubwa inayostahili kusherehekewa na wadau wa soka ya wanawake ulimwenguni kote kwa namna.

Kulingana naye, kikosi hicho kitafungua milango ya uchumi kwa wanasoka wengi wanaopania kujikuza kitaaluma.

Hegerberg, 24, alikuwa mshindi wa kwanza wa taji la mchezaji bora duniani kwa upande wa wanawake, Ballon d’Or mnamo 2018.

“Ni matumaini yetu kwamba Real watawekeza zaidi katika kikosi hiki na kukistawisha kwa kipindi kirefu ili kiwafae wanasoka wengi,” akaongeza Hegerberg.

Tacon iliyoanzishwa mnamo 2014, walijishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu ya Uhispania kwa upande wa wanawake mnamo 2019 wakifahamu uwezekano wa umiliki wao kubadilishwa.

Katika kipindi hicho, kikosi hicho kilisajili Kosovare Asllani na Sofia Jakobsson kutoka Uswidi na kiungo mzawa wa Brazil, Thaisa kutoka AC Milan ya Italia.

Asllani na Jakobsson wameteuliwa kuwa miongoni mwa wawaniaji wa taji la Ballon d’Or mnamo 2019-20.