Michezo

Ferguson Rotich aalikwa kunogesha mbio za Diamond League jijini Stockholm

August 14th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MKENYA Ferguson Rotich ni miongoni mwa wanariadha wa haiba kubwa ambao wamealikwa kushiriki mbio za Wanda Diamond League ambazo zimeratibiwa kufanyika Agosti 23 jijini Stockholm, Uswidi.

Ferguson aliibuka mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 800 kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini Doha, Qatar mnamo 2019.

Atanogesha tena mbio hizo nchini Uswidi huku akitazamiwa kumtoa jasho bingwa wa dunia Donavan Brazier wa Amerika na mshindi wa medali ya fedha duniani, Amel Tuka wa Bosnia.

Mwingine ambaye amethibitishwa kushiriki mbio hizo za mizunguko miwili mnamo Agosti 23 ni mshikilizi wa rekodi ya kitaifa nchini Uswidi, Andreas Kramer.

Kwa upande wa wanawake, Halima Nakaayi ya Uganda atafufua uhasama wake na Raevyn Rogers wa Amerika katika mbio za mita 800. Wawili hao walitawala fani hiyo katika Riadha za Dunia zilizoandaliwa Doha, Qatar mwaka jana kwa kuibuka katika nafasi ya kwanza na pili mtawalia.

Mwingereza Jemma Reekie anayejivunia muda bora zaidi wa binafsi wa dakika 1:57.91 pia atakuwa sehemu ya wanariadha watakaonogesha kivumbi hicho.

Licha ya changamoto tele ambazo zimezuliwa na janga la corona, waandalizi wa duru hiyo ya Diamond League mjini Stockholm, wamefanikiwa kuunga orodha ya wanariadha wa haiba kubwa watakaoibua msisimko zaidi miongoni mwa mashabiki.

Mondo Duplantis ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika fani ya urukaji ufito kwa upande wa wanaume, anatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki nchini Uswidi.

Atatoana jasho na Sam Kendricks aliyejizolea nishani ya fedha kwenye Riadha za Dunia mnamo 2019 na Piotr Lisek aliyeridhika na medali ya shaba. Bingwa wa Olimpiki Thiago Braz na Raphael Holzdeppe aliyeibuka mfalme wa dunia mnamo 2013 pia watakuwa sehemu ya washindani watakaopania kumlambisha sakafu Duplantis.

Bingwa wa dunia katika urushaji wa kisahani, Daniel Stahl atakuwa pia akilenga kusajili matokeo ya kuridhisha mbele ya mashabiki wa nyumbani. Atashindana na Andrius Gudzius aliyeibuka bingwa wa dunia mnamo 2017 na chipukizi wanaoinukia vyema zaidi nchini Slovenia na Uswidi – Kristjan Ceh na Simon Pettersson mtawalia.