HabariSiasa

Feri: Joho aahidi kuita waokoaji wa Afrika Kusini

October 2nd, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO

SHUGHULI ya kusaka gari lililotumbukia Jumapili katika Bahari Hindi ziliendelea jana huku Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho akiahidi kuleta wataalamu kutoka Afrika Kusini kusaidia katika shughuli hiyo.

Bw Joho ambaye alifika katika kivuko cha Likoni mara ya kwanza tangu mkasa huo utokee siku tano zilizopita, alitoa mchango wa Sh2 milioni kuifariji familia ya marehemu Miriam Kighenda.

“Serikali yangu itarudisha pesa ambazo familia hii ilitoa kulipa muokoaji wa kibinafsi. Niko tayari hata kuita waokoaji wenye uzoefu kutoka Afrika Kusini ili wasaidiane na hawa wetu,” akasema.

Bw Joho awali alilaumiwa na umati uliofurika katika kivuko hicho cha feri, wakidai alikosa kufika hapo mapema kuifariji familia.

Bw Joho aliwahakikishia wanafamilia pamoja na wakazi waliofika hapo kuwa hakuna atakayezuiwa kuchangia katika uopoaji huo.

Kauli yake ilijiri baada ya Msemaji wa Serikali, Kanali Mstaafu Cyrus Oguna kumtaka muokoaji wa kibinafsi Bw Musa Sila asishiriki katika shughuli hiyo, akidai kuwa amekuwa akitoa habari za kupotosha.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Shirika la Huduma za Feri, Bw Dan Mwazo alimtetea muokoaji huyo na kusema kwamba alikuwa amekatazwa kutumia mashua ya Jeshi la Wanamaji, ambayo ina uwezo mkubwa wa kutumika katika uokoaji huo.

Baadaye, Katibu Katika Wizara ya Uchukuzi na Miundo Msingi, Bi Esther Koimett alifika mahali hapo, na kuahidi kuwa umma utapata habari kamili kupitia kituo maalum kilichoanzishwa jana.

Usafiri ulisimamishwa kwa saa kadhaa wakati wa shughuli hiyo, jambo lililoudhi wasafiri waliobeba mabango ya kumkashifu Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Ferry, Bw Bakari Gowa, waliyedai ameshindwa kuwahakikishia usalama wanaotumia kivuko hicho.

Aidha, walimlaumu kwa kushindwa kurekebisha feri kuukuu ambazo zimekuwa zikisababisha ajali za mara kwa mara.

Maafisa wa usalama walipata wakati mgumu kutuliza rabsha hizo na ilibidi kutumia bunduki kutishia kundi hilo. Hatimae kundi hilo lilijipenyeza baada ya lango kufunguliwa kumruhusu Bw Joho kuwafariji familia ya wenda zao Bi Kighenda na mwanawe Diana Mutheu.

Bi Monica Wangare mama mlezi wa mwendazake Bi Kighenda alilaumu shirika la Kenya Ferry kwa kukosa vifaa vya uokoaji.