Habari

Feri tatu zapigwa marufuku kuhudumu Likoni

December 11th, 2019 1 min read

NA SAMWEL OWINO

TATIZO kubwa la uchukuzi lanukia katika kivuko cha feri Likoni, Kaunti ya Mombasa baada ya Bunge la Taifa kupitisha pendekezo lililotaka feri tatu zipigwe marufuku kuhudumu.

Ripoti ya kamati ya kuhusu Uwekezaji wa Umma iliyochunguza usalama wa wasafiri wanaotumia kivuko hicho, ilisema feri hizo ambazo zimehudumu kwa zaidi ya miaka 20 si salama kwa wasafiri.

Kufuatia hatua ya wabunge kukubali utekelezaji wa yaliyomo kwenye ripoti hiyo, Mamlaka ya Usafari wa Majini (KMA) sasa inatarajiwa kufutilia mbali leseni za feri zote ambazo hazijatimiza viwango vinavyohitajika vya usalama.

Ripoti ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir ilipata kuwa feri tatu zimehudumu kwa miaka 30 kinyume cha sera za Shirika la Huduma za Feri, ambazo zinasema kwamba chombo hicho cha usafiri kinafaa kubadilishwa baada ya miaka 20.

Ijapokuwa kuna feri sita kwa jumla, ni MV Harambee, MV Nyayo na MV Kilindini ambazo huhudumu wakati mwingi Likoni.

Feri nyingine zilizopo ni MV Likoni na MV Kwale ambazo zimetumika kwa miaka 10, na MV Jambo ambayo imehudumu kwa muda wa miaka miwili pekee.

Meneja Mkuu wa KFS, Bakari Gowa alithibitishia kamati hiyo mwezi Jumatano kwamba feri hizo tatu zimehudumu kupita muda uliowekwa kwenye sheria kwa sababu hawana fedha za kununua mpya.

“Shirika linalodhibiti huduma za majini (KMA) linafaa kuhakikishwa kwamba vibali vya kudumu vya feri ambazo si salama vimefutiliwa mbali,” ikasema ripoti hiyo.

Kwenye ripoti yao, wabunge hao walisema walijuzwa kwamba KMA ilikuwa imetambua hitilafu 12 kwenye MV Harambee kufikia Februari 2019.

“Hitilafu hizo zilichangia ajali ambapo gari liliteleza kutoka kwa MV Harambee mnamo Septemba 2019 na kusababisha vifo vya mama na bintiye,” ikaongeza ripoti hiyo.

Wakati uchunguzi wa wabunge ulipofanywa, ilibainika kwamba feri hizo zilikuwa na matatizo takriban 12 ambazo zinahatarisha maisha ya wasafiri.

Imekuwa kawaida kushuhudia feri zikikwama katikati ya bahari na kuanza kuyumbayumba baharini kwa muda kabla kuendeleza safari zake.