Habari Mseto

Feri: Wazee, familia watofautiana kuhusu tambiko

October 6th, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO

KULIKUWA na hali ya vuta nikuvute baina ya familia ya mwanamke aliyetumbukia baharini Miriam Kighenda na wazee Wadigo ambao wanasisitiza kuwa ni sharti matambiko yafanywe katika kivuko cha Likoni ili kuopoa miili huku familia hiyo ikishikilia kuwa kufanya hivyo ni kinyume na imani yao ya Kikristo.

Wazee hao walisisitiza kuwa tambiko la kumwaga damu ya mnyama katika sehemu hiyo linapaswa kutekelezwa ili kuridhisha majini wanaoishi katika bahari hiyo.

Mzee Mwinyihamisi Mwakinyasi alisema mapepo hao ndio wanaohusika na majanga yanayotokea katika kivuko hicho.

Aidha alidai kuwa inachukua waopoaji siku nyingi kukamilisha zoezi hilo kwa sababu mapepo hao wanazuia gari hilo ndani ya mapango yao.

“Chakula cha mapepo ni damu ya mnyama hususan ng’ombe mweusi, kufuatia kizazi kukumbatia usasa na hali ya uchumi, mila na tamaduni zimesahaulika, majanga haya yanatokea ili kutukumbusha wajibu wetu kama jamii,”alieleza.

Mzee huyo alidai kuwa awali sehemu hiyo ilitumiwa na wazee wa kidigo kutoa kafara mara kwa mara ili kuepuka majanga yanayosababishwa na mapepo wabaya.

Hata hivyo familia ya mwendazake ilikataa kuhusishwa na zoezi hilo wakisema kuwa imani yao ya dini ya Kikristo haiwaruhusu kutekeleza zoezi hilo.

Walisema wamehusisha wakuu wa kanisa kuombea miili ya Bi Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu ili kupata utulivu waliko na kujitokeza kwa haraka.

“Hatuamini tamaduni hizo, tukishiriki katika matambiko itakuwa tumeenda kinyume na maagizo ya dini yetu,tutaendelea kufanya maombi ili Mwenyezi Mungu apatie jeshi letu maarifa, uwezo na kuwafumbua macho waone miili ya wapendwa wetu,” alisema msemaji wa familia hiyo Bw Luka Mbati.

Askofu wa kanisa la ACK, Bw Julius Kalu, alikashifu kauli za wazee hao akisema Wakristo hawapaswi kuamini nguvu zaidi ya Yesu Kristo.

Alisema ni muhimu kwa familia ya mwenda zake kuja pamoja kufanya maombi ili kuitisha msaada kutoka kwa Mungu aliyewaumba.

Alieleza kuwa majini na pepo wote wachafu wanapaswa kukemewa na si kuridhishwa kwa makafara kama wanavyodai wazee hao.

“Hatupaswi kuabudu kiumbe chochote isipokuwa aliyetuumba, kuwatolea mapepo kafara itakuwa ni sawa na kuwatukuza jambo ambalo ni kinyume na dini yetu,” alisema.

Katibu mkuu wa muungano wa maimamu na wahubiri nchini Kenya Bw Sheikh Khalifa Mohammed alisema tukio hilo halihusiani kivyovyote na majini.

Alisema kuwa tukio hilo lilikuwa ajali kama nyingine hivyo wazee hao hawapaswi kupotosha familia ya mwenda zake.

Alisema kulingana na dini ya Kiislamu, watu hawafai kuchinja kwa jina lolote isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Aidha, alisema kutekeleza zoezi la matambiko ni makosa kwani ni kumkasirisha Muumba.

“Kufanya matambiko ni hatia kubwa sana, humtoa Muislamu katika dini,” alisema.

Wakati huo huo aliwaomba Wakenya kuungana na familia ya mwenda zake kwa maombi.

Zoezi la uopoaji linaendelezwa na shirika la utoaji huduma za feri (KFS), mamlaka ya bandari (KPA), kikosi maalum cha ulinzi baharini, (KCGS) na taasisi ya utafiti wa baharini.

Jumamosi ilikiwa ni siku ya saba tangu gari la Bi Kigenda kutumbukia majini baada ya kurudi nyuma likiwa ndani ya feri Jumapili iliyopita.