Habari

Feri zinazotumika nchini sio salama kwa usafiri, wakuu KFS waungama

October 29th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SHIRIKA la Feri Nchini (KFS) sasa limeungama kwamba feri zake zote sita hazijatimiza viwango vya usalama vinavyokubalika na shirika la kimataifa la kuidhinisha vyombo vya baharini, Lloyd Register Group Limited.

Mkurugenzi Mkuu wa KFS Bakari Gowa na Mhandisi Mkuu wa shirika hilo Peter Mathenge wamewaambia wabunge kwamba feri za kwanza kufutiliwa mbali kutoka kampuni ya Lloyd mnamo 2007 ni MV Harambee, MV Nyayo na MV Kilindi.

Hii ni kwa sababu zmetumika kwa miaka 30 ilhali kulingana na sheria feri zilipitisha miaka 20 hazipasi kuendelea kutumika.

Na feri za MV Jambo, MV Mvita na MV Kwale zimekuwa zikitumika ilhali hazijakaguliwa na shiriki hilo la kimataifa kubaini ikiwa ni salama kutumika.

Mbw Bakari na Mathenge pia Jumanne wamewaambia wanachama wa kamati ya bunge kuhusu uwekezaji (PIC) kwamba manahodha (coxswain) wanaohudumu katika feri hizo hawana vyeti vya kisasa vya uhitimu.

“Kimsingi, feri zetu zote hazijatimiza viwango hitajika kimataifa. Lakini tumekuwa tukizifanyia ukarabati kila mara kwa mara kuhakikisha kuwa zinatumika,” amesema Bw Gowa alipofika mbele ya kamati katika majengo ya bunge, Nairobi.

Salama

Ameiambia kamati hiyo, inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sheriff Nassir, kwamba Mamlaka ya Shughuli za Baharini (KMA) iliipa KFS idhini ya kuendelea kutumia feri hizo huku ikiendelea kuzifanyia “ukarabati kuhakikisha ni salama kwa uchukuzi.”

“Kando na hayo, tulitangaza mara tatu katika vyombo vya habari tukisaka manahodha waliohitimu katika kiwango cha kimataifa lakini mpaka sasa tumepata mtu mmoja pekee. Na uchunguzi wetu umebainisha kuwa humu nchini hakuna chuo cha mafunzo ya manahodha ambao tunahitaji,” akasema Bw Gowa.

Mkurugenzi Mkuu wa KFS Bakari Gowa (wa pili kushoto) na Mhandisi Mkuu wa shirika hilo Peter Mathenge (kushoto). Picha/ Charles Wasonga

Wasimamizi wa shirika la KFS wamekuwa wakihojiwa ikiwa ni muda wa mwezi mmoja baada ya mkasa kutokea katika kivuko cha Likoni ambapo Mariam Kighenda na bintiye Amanda Mutheu walikufa maji baada ya gari lao (walimokuwa ndani) kuteleza kutoka kwa feri ya MV Harambee na kutumbia baharini.

Gari hili liliopolewa baada ya siku 13 katika operesheni iliyoendeshwa na wapigambizi wa asasi za humu nchini ambao walipata usaidizi kutoka wataalamu kutoka Afrika Kusini.

Ni kutokana na mkasa huo ambapo wiki jana, Rais Uhuru Kenyatta aliwafuta kazi mwenyekiti wa Bodi ya Wasimamizi wa KFS Dan Mwazo na wanachama kwa utepetevu kazini.

Wabunge wamewasuta wasimamizi wa KFS kwa kutochukua hatua zozote za kuzifanyia ukarabati feri zake hata baada ya mkasa huo wa Likoni.

“Tuna nakala ya barua hapa ambayo mamlaka ya KMA ikiandikia KFS ikiishauri kuifanyia ukarabati feri hii ya MV Harambee ambayo iko katika hali mbaya. Je, mlipata barua hiyo?” Bw Nassir akauliza.

Bw Gowa ameungama kuwa ofisi yake ilipokea barua hiyo lakini akasema hawajaanza kuendesha kazi hiyo ya ukarabati kutokana na ukosefu wa fedha kutoka Wizara ya Fedha.

“Tukipata pesa wakati wowote kuanzia sasa, tutaanza ukarabati huo kulingana na maagizo ya KMA,” akasema.

Hata hivyo, haijabainika kama maelezo yao yamejikita tu kwa feri za Pwani nchini kwani pia ni muhimu kufahamu kwamba katika maeneo ya Nyanza, kuna feri inayohudumu baina ya Luanda K’Otieno katika eneobunge la Rarieda, Kaunti ya Siaya hadi Mbita, Kaunti ya Homa Bay.

Yapo maelezo kwamba feri ya Luanda K’Otieno ni ya mmiliki binafsi.