Fida-K yalalamikia ongezeko la mauaji ya wanawake Kenya

Fida-K yalalamikia ongezeko la mauaji ya wanawake Kenya

Na BENSON MATHEKA

SHIRIKISHO la mawakili wanawake nchini (Fida- Kenya), limeitaka serikali kulinda wanawake na wasichana na kukomesha mauaji ambayo yanaendelea kuongezeka nchini.

Maafisa wa chama hicho walisema uchunguzi wao umeonyesha kuwa, idadi ya visa vya mauaji ya wanawake inazidi kuongezeka nchini.

Wakilaani mauaji ya hivi majuzi ya naibu mkurugenzi wa Tume ya Ardhi (NLC) Jennifer Wambua na Velvine Kinyanjui, maafisa hao walisema serikali ina jukumu la kikatiba la kuwalinda wasichana na wanawake kutoka kwa wauaji.

“Idadi ya mauaji inatia wasiwasi na kama FIDA-Kenya tunasikitishwa na usalama wa wanawake na wasichana katika nchi hii. FIDA- Kenya inahimiza serikali kutekeleza jukumu lake la kulinda wasichana na wanawake dhidi ya mauaji,” alisema mwenyekiti wa FIDA- Kenya, Nancy Ikunu.

Mwili wa Bi Wambua ulipatikana katika kichaka eneo la Ngong siku kadhaa baada ya kutoweka, naye Bi Kinyanjui anadaiwa kuuawa na mwanamume aliyekuwa mpenzi wake.Bi Ikunu alisema uchunguzi wa FIDA- Kenya unaonyesha kuwa ghasia za kijinsia na kingono zinachangia mauaji ya wanawake.

“Haki na usalama wa raia wote ni jukumu la pamoja na ni juu yetu sote kutaka serikali kuwajibika katika kutekeleza haki zetu,” alisema.Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Ann Ireri, kuna kesi kadhaa kortini ambazo linataka serikali kuwajibika katika kulinda wanawake.

“FIDA-Kenya inawahimiza wanawake wanaokabiliwa na ghasia za kingono na jinsia kuchukua hatua kuhakikisha usalama wao: usisubiri hali kuwa mbaya zaidi. Tafuta usaidizi kupitia nambari yetu isiyotozwa malipo ya 0800 720 501,” alisema.

You can share this post!

Wakili Karim Khan kujiondoa kwenye kesi ya Ruto ICC

Mtambue ‘Kanini’ wa kipindi cha Maria