Habari Mseto

FIDA yalia dhuluma nyumbani zimezidi

December 16th, 2020 2 min read

Na WINNIE ATIENO

SHIRIKA la Mawakili Wanawake nchini – Fida – limelalamikia ongezeko la visa vya ubakaji, unajisi, vita vya nyumbani, visa vya wazazi kupigania watoto na akina mama kutaka pesa kukidhi mahitaji ya watoto wao wakati wa janga la corona.

Mnamo Aprili 15 Fida-Kenya ilizindua nambari ya huduma za dharura bila malipo ya 0800720501 na kufikia Novemba 30 ilikuwa imepokea kesi 5027. Idadi kubwa ya visa hivyo vikiwa ubakaji na unajisi, vita vya nyumbani na huduma za ushauri nasaha.

Bi Anne Ireri alisema Fida-Kenya imesikitishwa na ongezeko la visa vya dhuluma za kijinsia hasa katika maeneo ya Magharibi na Pwani wakati huu wa janga la corona. Maeneo mengine ni Nairobi na viunga vyake, huku kaunti ya Machakos ikirekodi idadi kubwa ya visa vya mimba za mapema.

“Mahitaji ya ushauri nasaha na afya ya akili yanajitokeza kutokana na msongo wa mawazo ulioshuhudiwa pakubwa wakati huu wa Covid-19. Tumekuwa mstari wa mbele katika kampeni ya afya ya kiakili wakati huu wa corona. Wakenya wamepata msongo wa mawazo kutokana na kupoteza kazi na mapato. Sasa tunaangazia jinsi Wakenya wanaweza kupata haki ili jamii isipate taabu,” alisema mkurugenzi wa Fida-Kenya Anne Ireri.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo cha haki kimtandao katika afisi zao mjini Mombasa, Bi Ireri alisema kuwa kutokana na kufungwa kwa shule, baadhi ya wasichana wanaendelea kupitia dhuluma za kijinsia.

“Baadhi yao wananajisiwa; jana tu tuliona katika vyombo vya habari baba aliwanajisi wanawe. Inahuzunisha na kusikitisha sana,” alilalamika Bi Ireri.

Ushirikiano

Ifikapo Januari, Fida-Kenya itashirikiana na Wizara ya Elimu kuhakikisha wasichana wote hata waliotungwa mimba wanarejea shuleni.

Bi Ireri alisema kuwa wasichana wote hata waliona na uja uzito ni sharti waruhusiwe kurejea shuleni ifikapo Januari mwakani bila ya kunyanyapaliwa wala kubaguliwa.

“Ifikapo Januari tutatoa ripoti yetu kufahamu ni wasichana wangapi wajawazito wamerejea shuleni na wanaendelea na masomo yao. Chini ya wizara hiyo, kuna sheria inayoruhusu wasichana wajawazito kurejea shuleni na tutakuwa makini kuona kuwa hatua zinachukuliwa ili kuhakikisha wasichana wanaendeleza masomo kama kawaida,” Bi Ireri alisisitiza.

Kufikia sasa Fida-Kenya imezindua vituo hivyo katika afisi zao za Nairobi na Kisumu.

Afisa anayesimamia shirika hilo eneo la Pwani Bi Ilhan Hisham alisema kuwa kituo hicho kitapiga jeki juhudi za wanawake na wasichana wanaotafuta haki.

Mkuu wa kituo cha mahakama ya watoto ya Tononoka Viola Yator alisema kuwa licha ya kwamba mahakama mtandaoni imewapiga jeki, wanakabiliwa na changamoto ikiwemo umeme kukatika mara kwa mara na pia huduma za intaneti.

Aliwataka wahisani wajitokeze kuwasaidia na tarakilishi na huduma za intaneti ili waweze kuweka hema nje ya mahakama kwa wateja wasio na mawakili waweze kujiwakilisha.