Habari Mseto

Fida yawashikisha adabu Aisha Jumwa na Edwin Sifuna

December 17th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO 

Shirikisho la Mawakili Wanawake nchini, Fida– Kenya, limewaonya wanasiasa dhidi ya kujihusisha katika dhuluma za kijinsia kufuatia mzozo ulioshuhudiwa kati ya Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna.

Wawili hao walirushiana cheche za matusi ambazo Fida imeonya kuwa ni dhuluma za kijinsia.

Katika kampeni za uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Mswambweni Bw Sifuna na Bi Jumwa walirushiana maneno makali hadharani ambayo Fida-Kenya ilionya kuwa ni matumizi ya maneno yenye kudunisha jinsia ambayo huenda yakazua uhasama.

Akizungumza mjini Mombasa mkurugenzi mkuu wa Fida-Kenya Bi Anne Ireri alisema kuwa matamshi ya wawili hao ni ya kutia wasiwasi kwani huenda watoto wakaiga matusi hayo.

“Tumeona mtindo wanaoutumia na ni jambo la kukera sana. Hili si swala la Msambweni pekee, ujumbe wetu kwa wanasiasa ni kwamba wawe makini na lugha wanayotumia kwenye kampeni haswa dhidi ya wapinzani wao. Kama Fida tumekerwa sana na utumizi wa lugha ya matusi na tunawataka wanasiasa wote kuheshimiana na kutotumia lugha za matusi. Tuwe vielelezo bora kwa jamii. Mswambweni iwe mwisho kwa matumizi ya matamshi ya kudunisha jinsia. Ubakaji sio jambo la utani,” alionya Bi Ireri.

Shirikisho la Mawakili Wanawake nchini Fida– Kenya limewaonya wanasiasa dhidi ya kujihusisha katika dhulma za kijinsia kufuatia mzozo ulioshuhudiwa kati ya mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna. Mkurugenzi mkuu wa Fida-Kenya Bi Anne Ireri. Picha/ Winnie Atieno

Alisema ni jambo la kusikitisha kuona watoto wakishuhudia jinsi wanasiasa wanavyorushiana matusi hadharani.

“Tukienda mbele tunataka kampeni za amani na heshima haswa tunapoelekea katika kampeni za BBI na uchaguzi mkuu. Tusifanye mzaha na maswala ya ubakaji au dhulma za kijinsia,” alisisitiza Bi Ireri.