HabariSiasa

Field Marshal Muthoni: Tusijidaganye kuwa tumepata uhuru

March 19th, 2018 3 min read

Na JOSEPH WANGUI

Kwa ufupi:

  • Field Marshal Muthoni asema hata Sh2,000 za kila mwezi kwa wazee walio na umri wa zaidi ya miaka 65 hapewi, wala hakupata fedha zilizotolewa na Uingereza kufidia wapiganaji wa Mau Mau
  • Asema kwamba Kenya bado inapambana na umaskini, ujinga, magonjwa, ukabila na wizi wa mali ya umma
  • Analalamika kwamba serikali ambazo zimekuwepo tangu 1963 zimewapuuza wapiganiaji wa uhuru ambao walijitoa dhabihu kwa kumwaga damu yao kwa ajili ya uhuru wa nchi hii
  • Anaeleza kuwa licha ya kupigania uhuru wa nchi hii kwa jino na ukucha, kitu pekee alichopewa na serikali ni jozi la viatu!

MWANAMKE pekee mpiganiaji uhuru aliyefikia cheo cha Field Marshal katika kundi la Mau Mau, Bi Muthoni Kirima amelalamika kuwa hajawahi kuonja matunda ya uhuru licha ya mchango wake kukomboa Kenya mikononi mwa wakoloni.

Kulingana na Field Marshal Muthoni, aliye na miaka 95, Kenya bado haijapata uhuru kamili na hakuna cha kusherehekea, sio tu kwa wapiganaji wa Mau Mau mbali kwa idadi kubwa ya Wakenya.

Aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano kuwa hata Sh2,000 za kila mwezi kwa wazee walio na umri wa zaidi ya miaka 65 hapewi, wala hakupata fedha zilizotolewa na Uingereza kufidia wapiganaji wa Mau Mau.

Katika kile anasema kinamkumbusha kuwa Wakenya bado hawajapata uhuru, Bi Muthoni hajawahi kunyoa nywele tangu alipoingia kichakani mnamo 1950 kujiunga na Mau Mau, na anasisitiza kuwa hatanyoa hadi Kenya ifikie kile anachosema ni uhuru kamili.

Field Marshal Muthoni Kirima, 81, alipokutana na Mama wa Taifa Bi Margaret Kenyatta katika hoteli ya Villa Rosa Kempinski, Nairobi awali. Picha/ Maktaba

“Nitakata nywele hizi wakati Kenya itapata uhuru wake kamili. Kwa sasa kuna machache sana ya kujivunia, miaka 54 tangu serikali ya Uingereza ilipoondoka hapa nchini na kuturuhusu tujitawale,” anasema Bi Muthoni.

Anasema wapiganaji wakiwa vitani walikubaliana kuwa wangenyoa nywele Kenya ikipata uhuru, lakini kulingana naye hayo bado hayajaafikiwa.

Anaamini Wakenya wengi hawajanufaika na uhuru uliopatikana 1963 na kwamba Wakenya wanaishi kwa njia ya kujindanganya kuwa yote yako sawa.

Anasema kwamba Kenya bado inapambana na umaskini, ujinga, magonjwa, ukabila na wizi wa mali ya umma.

Shujaa huyo alipewa cheo cha Field Marshall na aliyekuwa kiongozi wa wapiganaji wa Mau Mau, Field Marshal Dedan Kimathi ambaye alinyongwa na serikali ya mkoloni na kuzikwa pahali pasipojulikana Februari 18, 1957.

Bi Muthoni alikuwa akiongoza wapiganaji dhidi ya Waingereza akiwa katika msitu wa Aberdare, akiwa amejihami kwa bunduki mbili na upanga na alikuwa mwanamke pekee kiongozi wa vita msituni.

Wakati wa vita alijeruhiwa vibaya lakini hakuwahi kukamatwa na maafisa wa usalama wa Uingereza ambao walikuwa wakiwindana naye usiku na mchana kwa sababu ya ukakamavu wake.

Analalamika kwamba serikali ambazo zimekuwepo tangu 1963 zimewapuuza wapiganiaji wa uhuru ambao walijitoa dhabihu kwa kumwaga damu yao kwa ajili ya uhuru wa nchi hii.

Analaumu shida zake na za mamilioni ya Wakenya kwa viongozi ambao anasema wanaongozwa na tamaa ya kibinafsi.

“Wapiganaji bado wanaishi katika umasikini mkubwa, hawana ardhi na watoto wao ni maskini, hawana kazi wala elimu. Wale ambao hawakuwa katika vita na walishirikiana na wakoloni wana maisha mazuri wakati sisi tuliojitoa mhanga tunaishi katika maskini.

Field Marshal Muthoni Kirima, 81, mpiganiaji hodari wa uhuru. Yeye ndiye jemedari mwanamke pekee katika vita vya kukomboa Kenya dhidi ya ukoloni.
Picha/Bernadine Mutanu

Ndio sababu ninaamini kuwa bado hatujapata uhuru na mimi nitanyoa nywele wakati shida za wapiganiaji uhuru na Wakenya wengine zitashughulikiwa,” anasema.

Bi Muthoni anasimulia kuwa baada ya kusalimisha silaha zao kwa Serikali ya Mwafrika katika uwanja wa Ruring’u mjini Nyeri mnamo 1963, alifikiri kwamba ulikuwa mwanzo wa kufurahia matunda ya uhuru lakini hali haikuwa hivyo. Anaeleza kuwa kitu pekee alichopewa na serikali kilikuwa jozi la viatu.

Serikali hiyo pia iliamuru mpiganaji mmoja wa Mau Mau, Eliud Rware Ngunjiri, kuwa mlinzi wake. Mzee huyo mwenye umri wa miaka 85 bado anatumikia jukumu hilo hadi sasa, ingawa bila malipo yoyote.

Matarajio ya Bi Muthoni yalikuwa wapiganaji wangetuzwa kwa juhudi zao za kuikomboa nchi. Lakini matarajio hayo yalififia ndiposa akaamua kushiriki shughuli za biashara ili kujikimu kimaisha.

Bi Muthoni anasema  hakupata fedha zilizotolewa na Serikali ya Uingereza kufidia waliokuwa wapiganaji wa Mau Mau kwa makosa waliyotendewa wakipigana Kenya.

“Majina ya wapiganaji halisi yalitumiwa na watu ambao hawakuhusika katika vita kupata pesa. Niliitwa na wakili mmoja mjini Nairobi aliyekuwa akifuatilia kesi yetu Uingereza lakini sikupata chochote,” anasema.

“Huo ulikuwa unyanyasaji na nilihisi nimetumika vibaya. Wale watu unaowaona wakikutana na viongozi wakidai ni waakilishi wa wapiganaji wa Mau Mau sio halali na hutumia majina yetu kupata fedha kwa ulaghai,” anasema Bi Muthoni huku akilia.