Michezo

Fifa kuipa Kenya Sh100 milioni kuinua soka ya vipusa

October 23rd, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKIKISHO la Soka la Kenya (FKF) limefichua kwamba Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) linapanga kuipa Sh101,210,000 za Kenya kuimarisha soka ya wanawake baada ya kuridhishwa na mipango yake.

Rais wa FKF Nick Mwendwa amesema jijini Nairobi mnamo Oktoba 23, 2018 kwamba Fifa imeamua kutengea Kenya fedha hizo baada ya kuiona inachukulia soka ya wanawake kwa uzito.

“Fifa imekuwa ikifuatilia soka ya Kenya kwa karibu. Imesema imefurahishwa na juhudi tunazofanya kuinua soka ya wanawake. Imetambua Kenya kama mojawapo ya mataifa yanayotilia mkazo zaidi katika uimarishaji wa soka ya wanawake.

Imeahidi kuwekeza Dola milioni moja za Marekani (Sh101,210,000 za Kenya) katika kipindi cha mwaka mmoja ama mwaka mmoja na nusu kijacho ili kufanikisha miradi ya kuinua soka ya wanawake,” Mwendwa ameambia vyombo vya habari jijini Nairobi.

Aidha, Mwendwa amesema kwamba Kenya itawekeza sehemu ya fedha hizo katika kufundisha makocha wa timu za kinadada. “Tuna tatizo kubwa humu nchini la kupata makocha wanawake. Sehemu ya fedha hizi itatumika katika shughuli ya kuwafundisha na kuwakuza makocha wanawake.”

Idadi kubwa ya klabu za wanawake nchini Kenya zinapata mafunzo kutoka kwa makocha wanaume. Hata timu ya taifa ya Harambee Starlets, ambayo imefuzu kushiriki Kombe la Afrika (AWCON) nchini Ghana mwezi ujao, iko chini ya kocha mwanamume – David Ouma