Michezo

FIFA yaangushia Chelsea, FA viboko kuhusu usajili wa 'watoto'

February 23rd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Soka Duniani (Fifa) limepiga klabu ya Chelsea marufuku kununua wachezaji katika vipindi viwili vijavyo vya uhamisho kama adhabu ya kusaini watoto.

Inamaanisha kwamba Chelsea haitaweza kusuka kikosi chake hadi mwisho wa Januari mwaka 2020. Mbali na adhabu hiyo, Chelsea pia imetozwa faini ya Sh60 milioni na kuamrishwa kuweka sawa hali ya wachezaji chipukizi wahusika katika siku 90 zijazo kuanzia Februari 22, 2019.

Shirikisho la Soka nchini Uingereza (FA) pia limejipata pabaya kwa kuvunja sheria za kusajiliwa kwa makinda.

Limetozwa faini ya Sh51 milioni na kuagizwa na FIFA kuhakikisha mikakati yake inayohusu uhamisho wa wachezaji wa kigeni pamoja na kusajiliwa kwa chipukizi iko sawa.

Kocha Maurizio Sarri wa klabu ya Chelsea. Picha/ AFP

“Kamati ya Nidhamu imeadhibu Chelsea kwa kuipiga marufuku kutosajili wachezaji wapya katika kiwango cha kitaifa na kimataifa kwa vipindi viwili vijavyo vya uhamisho,” taarifa kutoka FIFA imesema Ijumaa.

Marufuku hii haizuii Chelsea kuruhusu mchezaji kuhamia klabu nyingine na haiathiri timu ya wanawake ya Chelsea na ile ya futsal.

Rufaa

Chelsea ina siku tatu kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa FIFA ambayo ilichukua hatua hiyo baada ya kuchunguza klabu hii kuhusu kusajiliwa kwa wachezaji wa kigeni walio chini ya umri wa miaka 18 akiwemo mshambuliaji wa zamani Bertrand Traore kutoka Burkina Faso ambaye sasa ni mchezaji wa Lyon katika Ligi Kuu ya Ufaransa.

Traore alinunuliwa na Chelsea mwaka 2013 akiwa na umri wa miaka 18, ingawa hakusajiliwa hadi Januari mwaka 2014.

Tovuti ya Mediapart nchini Ufaransa imenuku stakabadhi kutoka kwa Football Leaks ikisema FIFA ilichunguza sajili 19 zilizofanywa na Chelsea kabla ya kufikia uamuzi wake.