Michezo

FIFA yachunguza baadhi ya wanasoka wa Kenya kuhusu madai ya kupanga matokeo ya mechi za Ligi Kuu

November 23rd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka Duniani (FIFA) limeanza kuwachunguza baadhi ya wachezaji na maafisa wa klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya Kenya ili kubaini kiwango cha kukithiri kwa matukio ya upangaji wa mechi za kipute hicho.

Kitengo cha Maadili cha FIFA kimekuwa kikiendesha uchunguzi wake kuhusiana na suala hilo na kikapiga marufuku wanasoka wanne wa kikosi cha Kakamega Homeboyz baada ya kuwapata na hatia ya kupanga matokeo ya mechi mbalimbali za Ligi Kuu ya Kenya hapo awali.

Huku Moses Chikati, Festo Omukoto na Festus Okiring wakipigwa marufuku ya miaka minne, George Mandela ambaye ni raia wa Uganda, alipokezwa adhabu kali zaidi baada ya kupigwa marufuku ya maisha. Nyota huyo wa zamani wa Kakamega Homeboyz sasa hatatakiwa kujihusisha na masuala ya soka katika maisha yake yote.

Katika sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu kuwepo kwa ulaghai wa upangaji wa matokeo ya mechi za Ligi Kuu ya Kenya, FIFA inatarajiwa kuanza kuwahoji baadhi ya wanasoka na maafisa wa vikosi mbalimbali kuanzia Novemba 23, 2020.

Kikosi cha Zoo FC kitakuwa cha kwanza baada ya kocha wao Herman Iswekha, mkufunzi wa zamani Sammy Okoth pamoja na mmiliki na mwenyekiti Ken Ochieng kuarifiwa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kujiwasilisha katika makao makuu ya shirikisho hilo, Kandanda House kwa minajili ya kuhojiwa na maafisa wa FIFA.

Wanasoka wa zamani wa Zoo FC – Sammy Sindani, Vincent Misikhu, Martin Elungat na Johnstone Ligare pia wametakiwa kujiwasilisha kwa mahojiano zaidi katika ofisi za FKF.

“FKF imepokea mawasiliano kutoka kwa FIFA kuhusiana na madai ya kuwepo kwa matukio ya upangaji wa matokeo ya baadhi ya mechi za Ligi Kuu ya Kenya. FIFA imeomba FKF kushirikiana nao kufanikisha uchunguzi huo kadri wanavyopania kuhoji baadhi ya wachezaji, makocha na maafisa wa soka wanaohusika na kabumbu ya Kenya. FIFA inaomba FKF iwape maafisa wake afisi za kutumia kwa minajili ya shughuli hiyo na kuwaalika waliotajwa katika barua hii kwa mahojiano zaidi,” ikasema sehemu ya barua iliyopokelewa na FKF kutoka FIFA na kutiwa saini na Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF, Barry Otieno.

Kwa mujibu wa mdokezi wetu kutoka FKF, wachezaji na maafisa wa vikosi vingi wamealikwa kwa mahojiano hayo yatakayoendeshwa na FIFA kwa wiki moja ijayo.

Nyota wa zamani wa Harambee Stars, George ‘Wise’ Owino ndiye mwanasoka wa kwanza wa haiba kubwa kuwahi kupigwa marufuku na FIFA kwa hatia ya kushiriki upangaji wa matokeo ya mechi mbalimbali za timu ya taifa ya Kenya mnamo 2019.

Beki huyo alipigwa marufuku ya miaka 10 na kutozwa faini ya Sh2 milioni kwa kushirikiana na mpangaji maarufu wa matokeo za mechi, Wilson Raj Perumal.

Owino ndiye alimtambulisha Mark Danyi kwa mmiliki wa Zoo FC, Ken Ochieng. Danyi ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Hungary aliyewahi kushirikiana na Perumal kupanga matokeo ya mechi mbalimbali.

Danyi aliwahi kujaribu kutwaa umiliki wa Zoo FC mapema katika mwaka wa 2019 kwa kutumia jina la kampuni ghushi ya TSMC Sports Consultancy.