Michezo

FIFA yakubali pendekezo la wachezaji 5 wa akiba

July 21st, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

VIKOSI kwa sasa vitaweza kuendelea kuwajibisha hadi wanasoka watano wa akiba hadi mwishoni mwa msimu ujao wa 2020-21 baada ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kurefusha kipindi cha kuwepo kwa sheria hiyo.

Kwa mujibu wa FIFA, sasa yatakuwa maamuzi ya ligi husika duniani na wasimamizi wa mapambano mbalimbali kuteua iwapo wangependa kuendelea kutekeleza sheria hiyo katika kampeni zao binafsi.

Kwa kuwa sheria hiyo itakuwepo hadi Agosti 2021, ina maana kwamba vinara wa kipute cha Euro 2021 na Copa America 2020 watakuwa na uhuru wa kuikumbatia katika kampeni zao zijazo au kuipuuza kabisa.

“Maslahi ya wachezaji ndiyo yaliyozingatiwa zaidi na FIFA katika maamuzi ya kuidumisha sheria hiyo hata katika kampeni za muhula ujao. Baadhi ya klabu zilizorejelea vipute vya msimu huu wa 2019-20 kwa kuchelewa zitahitaji muda zaidi za kupumzisha wanasoka wao ambao pia watahitaji likizo ya kutosha kadri watakavyopania kujiandaa kwa msimu mpya,” ikasema sehemu ya taarifa ya FIFA.

“Katika mashindano mbalimbali ya msimu wa 2020-21, mechi nyingi zitasakatwa kwa kurundikwa katika kipindi kifupi. Hii ni kwa sababu mapambano mengi yatachelewa kuanza na patakuwepo na ulazima wa kampeni hizo kutamatika mapema ili kupisha vipute vingine vya kimataifa kama vile Euro 2021, Copa America na mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar,” ikaendelea taarifa hiyo.

Maamuzi ya kuongeza idadi ya wachezaji wa akiba walio na uwezo wa kuwajibishwa katika mechi moja kutoka watatu hadi watano yalifanywa wakati shughuli za soka zilipokuwa zimesitishwa kote duniani kwa sababu ya janga la corona. Lengo kuu la sheria hiyo ni kuwaepushia wachezaji uwezekano wa kupata majeraha ya mara kwa mara.

Sheria hiyo imekuwa ikitumika katika soka ya Uingereza tangu kurejelewa kwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Juni 17, 2020 baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miezi mitatu.

FIFA imeshikilia kwamba timu zitaendelea kuwa na fursa tatu pekee za kufanya mabadiliko hayo ya hadi wachezaji watano katika mechi moja ili kutoharibu muda wa mapambano.