Michezo

Fiji madume wa raga duniani, Kenya mkiani

June 2nd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

FIJI ndiyo mabingwa wa Raga ya Dunia ya wachezaji saba kila upande ya msimu 2018-2019 baada ya kufunga kampeni yake kwa kuzoa taji la Paris Sevens kwa kubwaga New Zealand 35-24 nchini Ufaransa, Jumapili.

Taji hili la Raga ya Dunia ni la nne la Fiji waliotamba pia msimu 2005-2006, 2014-2015 na 2015-2016. Ni mara ya kwanza kabisa wanavisiwa hawa wametawala duru ya Ufaransa tangu ijumuishwe kwenye Raga ya Dunia mwaka 2000, ingawa waliwahi kutwaa mataji ya Ufaransa mwaka 1996 na 1997 yakiwa ya mwaliko.

Mbali na kuwa mabingwa wa Raga ya Dunia msimu 2018-2019, ambao ulikuwa wa 20, Fiji pia ilifuzu kushiriki Olimpiki nchini Japan mwaka 2020. Vilevile, nambari mbili Mareakni, tatu New Zealand na nne Afrika Kusini zilijikatia tiketi ya kushiriki Olimpiki kwa kumaliza Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 katika nafasi nne za kwanza.

Kenya, ambayo ilimaliza makala ya msimu 2017-2018 katika nafasi ya nane kwa rekodi yake ya alama 104, msimu huu ilitamatisha na alama 37 katika nafasi ya 13. Shujaa ya kocha Paul Murunga ilihitaji duru ya mwisho jijini Paris kujinasua kutoka hatari ya kutemwa. Imekuwa katika ligi hii ya mataifa 15 tangu msimu 2002-2003.

Msimamo wa Paris Sevens:

1.Fiji, 2.New Zealand, 3.Afrika Kusini, 4.Marekani, 5.Ufaransa, 6.Samoa, 7.Argentina, 7.Kenya, 9.Canada, 10.Ireland, 11.Australia, 11.Uingereza, 13.Scotland, 14.Japan, 15.Uhispania, 15.Wales

Msimamo wa Raga ya Dunia msimu 2018-2019:

1.Fiji (alama 186) – mabingwa

2.Marekani (177)

3.New Zealand (162)

4.Afrika Kusini (148)

5.Uingereza (114)

6.Samoa (107)

7.Australia (104)

8.Ufaransa (99)

9.Argentina (94)

10.Scotland (72)

11.Canada (59)

12.Uhispania (49)

13.Kenya (37)

14.Wales (31)

15.Japan (27) – imetemwa