Na JOHN KIMWERE
NI kati ya chipukizi wanaopania kufanya makubwa katika tasnia ya burudani miaka ijayo.
Tasnia ya uigizaji nchini inazidi kuimarika kinyume na miaka iliyopita hali ambayo imevutia wasanii wengi tu wanaoibukia.
Loreen Tesoti Chepkurui anasema ingawa ndio ameanza kupiga ngoma anatamani sana kuwa produsa mahiri katika masuala ya uigizaji nchini. ”Ninapenda kuigiza ingawa tangia nikiwa mtoto nilidhamiria kuhitimu kuwa mwanasheria. Katika tasnia ya uigizaji ninataka kufikia hadhi ya msanii Viola Davis mzawa wa Marekani.
Binti huyu aliyezaliwa mwaka 2002 anasema anapenda sana filamu yake iitwayo ‘Lila and Eve’.
Pia anadokeza kuwa alishawishika kujiunga na uigizaji baada ya kutazama filamu ya Monica aliyoshiriki Brenda Wairimu aliye kati ya waigizaji sifika nchini. Ingawa hajapata mashiko katika tasnia ya uigizaji anashikilia kuwa maigizo ni ajira inayolipa kama zingine.
Anajivunia kushiriki filamu kadhaa tangia aanze kujituma kwenye masuala ya uigizaji miaka minne iliyopita.
Ameshiriki filamu kama Varshita, Heaven is for humble, Makovu, Country Queen kati ya zingine. Varshita iliyotengenezwa na Moonbeam Production huonyeshwa kupitia Maisha Magic East.
Kwa jumla amefanya kazi na makundi mawili Koch Chocolate City na Moon Beam Production.
Binti huyu anasisitiza kuwa kazi yake kwenye filamu hizo inamtia motisha zaidi anaamini ana uwezo wa kufanya vizuri katika maigizo. Binti aliyezaliwa katika familia ya watoto wanne akiwa kitinda mimba anasema katika familia yao hakuna aliyejihusisha na masuala ya uigizaji.
Dada anasema huku nchini anapenda kufanya kazi na Kate Actress ambaye ameshiriki kipindi cha Mother inlaw kiliokuwa kikipeperushwa kupitia Citizen TV.
Kwa waigizaji wa kimataifa anasema anapenda sana kujikuta jukwaa moja na msanii wa Afrika Kusini, Sindiswa Dlathu na Mercy Johnson (Nigeria) walioshikiri filamu kama Muvhango na Hustlers mtawalia.
Changamoto
Ni msichana mdogo lakini inaonekana team mafisi hawafahamu hilo.
”Kusema ukweli kwa wanawake warembo hilo wanakutana nalo,” akasema na kutoa wito kwa wenzake kutokubali kushushwa hadhi na wanaume sampuli hiyo.
”Sina shaka kushauri wasanii wanaokuja kuwa ni muhimu kuheshimiana na kusaidiana panapohitajika badala ya kukomoana,” alisema na kuongeza baadhi ya waliotangulia wamekuwa na mtindo wa kujaribu kuzima ndoto za wenzao wanaoibukia.
Anashauri wana dada wanaoibukia kuwa wasiwe na pupa ya kupata umaarufu katika tasnia ya maigizo. Anasema itakuwa vyema kwa wanadada kuwakwepa wanaume ambao hupenda kuwashusha hadhi kwa kuwataka kimapenzi ili kuwapa ajira.
Aidha anawahimiza kuwa nyakati zote wanastahili kujiheshima pia kumweka Mungu mbele kwa chochote wanachofanya.