Michezo

Filip Krovinovic atua West Brom kwa mkopo

September 30th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

WEST Bromwich Albion wameafikiana na Benfica na kurefusha mkataba wa kiungo Filip Krovinovic, 25, kwa mwaka mmoja zaidi.

Mwanasoka huyo mzawa wa Croatia alihudumu kambini mwa West Brom kwa mkopo mwingine wa mwaka mmoja msimu uliopita wa 2019-20.

Katika kipindi hicho, aliwajibishwa mara 40 na akafunga mabao matatu. Alichangia sana ufanisi wa kupandishwa ngazi kwa West Brom hadi Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

“Najua maamuzi ya kusalia West Brom hayakuwa mepesi. Ndiposa mchakato mzima ukawa mrefu kiasi hicho. Hata hivyo, ni fahari tele kuendelea kuchezea kikosi hiki ambacho kimeonyesha imani kubwa kwangu,” akasema.

“Nilimweleza kakangu kwamba hii hatua ya kurefusha muda wa kuchezea West Brom ni sawa na kurejea shuleni baada ya likizo ndefu nyumbani. Kisha unakutana upya na marafiki zako na kuelezana mambo mengi,” akasema Krovinovic.

West Brom wameanza msimu wao mpya katika EPL kwa kupokea vichapo viwili na kuambulia sare ya 3-3 dhidi ya Chelsea uwanjani The Hawthorns licha ya kuongoza mechi hiyo kwa 3-0 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza.

Walisajili ushindi wa 3-0 dhidi ya Harrogate Town kwenye raundi ya pili ya Carabao Cup kabla ya kupepetwa 5-2 na Everton katika gozi la EPL mnamo Septemba 19 ugani Goodison Park.

Baada ya kupepetwa 3-0 na Leicester City katika mechi ya kwanza ya EPL msimu huu, West Brom walibanduliwa na Brentford kwenye raundi ya tatu ya Carabao Cup kwa mabao 5-4 kupitia penalti. Mechi hiyo iliikamilika kwa sare ya 2-2 mwishoni mwa dakika 90.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO