Fimbo ya maaskofu yawaumiza

Fimbo ya maaskofu yawaumiza

Na CECIL ODONGO

MARUFUKU ya kutozungumza siasa makanisani ambayo ilitolewa na baadhi ya viongozi wa kidini imeanza kuwaumiza wanasiasa wakuu nchini akiwemo Naibu Rais, Dkt William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Maaskofu wa makanisa ya PCEA, Katoliki na Anglikana mwanzoni mwa mwezi huu walipiga marufuku wanasiasa kuzungumza siasa ndani ya kanisa na badala yake kuwashauri waruhusu ibada imalizike kisha waandae mikutano yao na kuendeleza siasa zao nje ya jengo takatifu.

Askofu wa Kanisa la Kianglikana, Jackson Ole Sapit alikuwa wa kwanza kukumbatia marufuku hiyo alipowazima Bw Odinga, mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi na viongozi wengine kuzungumzia siasa wakati wa kutawazwa kwa Askofu Mpya wa Dayosisi ya Butere, Rose Okeno mnamo Septemba 12.

Marufuku hiyo, pamoja na nyingine za maaskofu wa Katoliki na awali ya kanisa la PCEA, inaonekana kuwaumiza Dkt Ruto na Bw Odinga ambao sasa wamekimbilia makanisa madogo ambako wanashiriki ibada kisha kutua kwenye miji ya karibu kuhutubia umati.

Hapo jana, Dkt Ruto akiwa katika kanisa la AIPCA, Timau, Kaunti ya Meru, aliyarai makanisa makuu nchini yalegeze ‘fimbo’ yao dhidi ya viongozi wa kisiasa ili “wale ambao wamegutuka sasa kuwa kuna mambo mazuri kanisani waruhusiwe kuhutubia waumini”.

Dkt Ruto alionekana hasa kumlenga Bw Odinga ambaye amekuwa akipinga michango ya fedha ambayo Naibu Rais alikuwa akiandaa ili kuyasaidia makanisa mbalimbali nchini.

Kauli ya Dkt Ruto ilichochewa na tamko la Askofu wa AIPCA, Samson Muthuri kuwa kanisa hilo si kati ya yale ambayo yamewawekea marufuku wanasiasa kutozungumza makanisani.

“Kuna baadhi ya watu ambao sasa wamegutuka na wanaona umuhimu wa makanisa nchini. Haitakuwa haki iwapo viongozi wa makanisa watawazuia kuzungumza altarini. Waruhusiwe waje wafahamu neno la Mungu,” akasema Dkt Ruto.

Mbali na AIPCA, Kanisa la Methodist pia limekuwa likiwaalika wanasiasa na kuwaruhusu kuhutubu bila kuwawekea marufuku yoyote.

Alimshukuru Askofu Muthuri pamoja na uongozi wa kanisa hilo kwa kutofuata makanisa mengini huku akitoa wito kwa makanisa ya PCEA, Katoliki na Kianglikana kubatilisha marufuku iliyopo.

Dkt Ruto hasa alikuwa akitumia majukwaa kanisani kumshambulia Bw Odinga huku akijipigia debe kurithi kiti cha urais 2022, pale Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu.

Katika Kaunti ya Laikipia, Bw Odinga naye alipewa fursa ya kuhutubu katika kanisa la PCEA, Nanyuki ila akazungumza tu maneno ambayo yanahusu umoja wa nchi. Bw Odinga alinukuu Zaburi 133 kushadidia kauli yake ya kusisitiza umoja wa nchi.

Waziri huyo Mkuu wa zamani amekuwa akiandaa vikao vya kieneo kuendeleza ajenda yake ya Azimio la Umoja

“Lazima tuungane kuhakikisha kuna umoja wetu hasa wakati huu ambapo tunakaribia uchaguzi mkuu. Ninatumia jukwaa hili kuwarai Wakenya wafuatilie maono ya waanzilishi wa taifa hili ya amani na umoja itawale miongoni mwetu,” akasema Bw Odinga.

Aidha, mnamo Ijumaa, Bw Odinga alikutana na waumini wa kanisa la Akorino mjini Gilgil katika Kaunti ya Nakuru ambapo alieleza kuwa kutakuwa na ukuaji wa uchumi tu iwapo taifa hili litakuwa na umoja.

Hatua ya Dkt Ruto na Bw Odinga kukimbilia makanisa madogo inafasiriwa kuwa njia ya kupata mwanya zaidi kuendeleza siasa zao kwenye mimbari.

You can share this post!

Nacada yalilia kituo cha kurekebisha tabia

Meru kuendelea kufaidi mradi wa kuboresha kilimo cha viazi