Firat ataja kikosi cha Harambee Stars kumenyana na Iran kirafiki jijini Tehran

Firat ataja kikosi cha Harambee Stars kumenyana na Iran kirafiki jijini Tehran

Na GEOFFREY ANENE

Harambee Stars itaingia kambini hapo Machi 17 kujiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa zamani wa Bara Asia Iran mjini Tehran hapo Machi 28.

Kocha Mturuki Engin Firat ametaja kikosi cha wachezaji 34 wakiwemo mshambulizi tegemeo Michael Olunga kutoka Al Duhail, kipa Ian Otieno (Zesco, Zambia), beki Joseph Okumu (Gent, Ubelgiji) na kiungo Kenneth Muguna (Azam, Tanzania), lakini hakuna nafasi kwa kiungo wa CF Montreal Victor Wanyama.

Beki wa kupanda na kushuka Eric Ouma kutoka AIK nchini Uswidi na mvamizi matata Benson Omalla anayeongoza ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Kenya, pia wapo pamoja na sura mpya Alfred Scriven kutoka IL Hodd, Norway, na mzawa wa Denmark Daniel Anyembe (Viborg).

Firat amesema kuwa winga Eric Johana kutoka Muangthong United nchini Thailand na mshambulizi Jonah Ayunga (St Mirren, Scotland) walikuwa katika mipango yake, lakini wako nje kwa sababu wamejeruhiwa.

“Tunasubiri kwa hamu kuona vijana, kufahamu wanavyoendelea na kuanza kuwa na mshikamano. Hatujakutana kwa zaidi ya siku 500,” Firat akasema.

Ameongeza, “Tunahitaji mfumo mzuri wa kutafuta wachezaji kutoka nje ya taifa wanaoweza kuchezea Kenya na kuwashawishi mapema. Baadhi ya wachezaji hao wamechezea timu za taifa barani Ulaya katika viwango vya chipukizi kwa hivyo kimchezo na kiakili wako tayari. Mataifa mengine Afrika yanafanya hivyo na tunahitaji kufuata mkondo huo.”

Kenya na Iran zimewahi kukutana mara mbili katika historia yao. Katika michuano hiyo ya kirafiki iliyochezewa ugenini, Kenya ilipoteza 3-0 Aprili 21, 1997 na kulemewa 1-0 Machi 18, 2009.

Iran, ambao wameshiriki Kombe la Dunia mara sita ikiwemo katika makala ya mwaka jana nchini Qatar, wanakamata nafasi ya 24 kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) nao Kenya wanapatikana katika nafasi ya 101.

Stars itakuwa ikisakata mechi ya kwanza ya kimataifa tangu ichape Rwanda 2-1 Novemba 15, 2021 katika mechi yake ya mwisho ya kutafuta tiketi ya Kombe la Dunia 2022. Ilipigwa marufuku na FIFA kabla ya marufuku hiyo kuondolewa Novemba 2022.

Kikosi cha Harambee Stars:

Makipa – Patrick Matasi (Police FC), Ian Otieno (Zesco, Zambia), Bryne Odhiambo (KCB), Levin Opiyo (AFC Leopards);

Mabeki – Joseph Okumu (Gent, Ubelgiji, Brian Mandela (Afrika Kusini), Johnstone Omurwa (Estrela, Ureno), Eric Ouma (AIK, Uswidi), Andrew Juma (Bandari), David Ochieng (Mathare United), Maurice Owino (KCB), Collins Shichenje (AIK, Uswidi), Mohamed Siraj (Bandari), Daniel Anyembe (Viborg, Denmark), Daniel Sakari (Tusker), Abud Omar (Police FC);

Viungo – Amos Nondi (Ararat, Armenia), Richard Odada (Philadelphia Union, Amerika), Teddy Akumu (Sagan Tosu, Japan), Alpha Onyango (Gor Mahia), Joseph Mwangi (Nzoia Sugar), Kenneth Muguna (Azam, Tanzania), Abdallah Hasan (Bandari), Duke Abuya (Police FC), Wilkims Ochieng (FC Koper, Slovenia), Moses Mudavadi (Kakamega Homeboyz), Alvin Mang’eni (Police FC), Hassan Beja (Nzoia Sugar), Victor Omune (AFC Leopards);

Washambulizi – Benson Omalla (Gor Mahia), Elvis Rupia (Police FC), Michael Olunga (Al Duhail, Qatar), Masud Juma (mkopo katika Al-Faisaly, Saudi Arabia kutoka kwa Difaa Hassani El Jadidi, Morocco), Alfred Scriven (IL Hodd, Norway).

  • Tags

You can share this post!

Raila asijaribu kuzua vurugu wakati wa maandamano, Ruto...

Ashtakiwa kwa kutaka kumuua dadake Raila

T L