Firat atatangaza kikosi cha Harambee Stars kusafiri Morocco kuvaana na Mali mchujo wa kuingia Kombe la Dunia

Firat atatangaza kikosi cha Harambee Stars kusafiri Morocco kuvaana na Mali mchujo wa kuingia Kombe la Dunia

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Mturuki Engin Firat ametaja kikosi chake cha mwisho cha Harambee Stars kitakachovaana na Eagles ya Mali kwenye mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 nchini Morocco mnamo Oktoba 7.

Mshambuliaji wa klabu ya Al Duhail, Michael Olunga, ambaye ni nahodha, ataongoza utafutaji wa mabao akisaidiana na mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Kenya msimu uliopita Eric Kapaito aliyenunuliwa na Arba Minch City nchini Ethiopia mwezi uliopita pamoja na chipukizi Henry Meja anayetarajiwa kujiunga na klabu ya AIK nchini Uswidi mwezi Januari 2022.

Joash “Berlin Wall” Onyango kutoka Simba SC nchini Tanzania, kipa Farouk Shikalo wa KMC nchini Tanzania na kiungo Ismael Gonzalez anayecheza soka ya malipo nchini Uhispania, ni baadhi ya majina yanayorejea kikosini baada ya kukosa sare tasa dhidi ya Uganda na 1-1 dhidi ya Rwanda mwezi uliopita.

Waliotemwa kutoka kikosi cha 34 waliotajwa Septemba 29 ni kipa James Saruni (Ulinzi Stars), mabeki Samuel Olwande (Kariobangi Sharks), Frank Odhiambo (Gor Mahia), Patila Omoto (Kariobangi Sharks), Keagan Ndemi (Bandari), Reagan Otieno (KCB), Musa Masika (Wazito) na mshambuliaji Sydney Lokale (Kariobangi Sharks). Ovella Ochieng hakuachiliwa na klabu yake ya Marumo Gallants, Afrika Kusini.

Stars imeratibiwa kusafiri nchini Morocco mnamo Oktoba 4 usiku. Mchuano huo utachezewa ugani Agadir kabla ya marudiano uwanjani Nyayo jijini Nairobi mnamo Oktoba 10.

Mali inaongoza Kundi E kwa alama nne baada ya kuchapa Rwanda 1-0 na kutoka 0-0 dhidi ya Uganda katika mechi zake mbili za kwanza. Kenya na Uganda zinafuatana katika nafasi ya pili na tatu mtawalia kwa alama mbili nayo Rwanda inavuta mkia kwa alama moja.

Kikosi cha Harambee Stars kinachosafiri Morocco:

Makipa – Ian Otieno, Brian Bwire, Faruk Shikalo;

Mabeki – Joseph Okumu, Joash Onyango, David Owino Odhiambo, Johnstone Omurwa, Eugene Asike, Daniel Sakari, David Owino Ambulu, Abud Omar, Eric Ouma, Bolton Omwenga;

Viungo – Richard Odada, Lawrence Juma, Ismael Gonzalez, Kenneth Muguna, Duke Abuya, Boniface Muchiri, Eric Zakayo, Phillip Mayaka, Abdalla Hassan;

Washambuliaji – Michael Olunga, Henry Meja, Eric Kapaito.

You can share this post!

WASONGA: Chiloba, wenzake wasaidie IEBC kufanikisha kura...

Rennes wapiga PSG breki kali katika kampeni za Ligue 1