‘Firirinda’ yapata umaarufu wa kipekee lakini mtunzi amesalia maskini

‘Firirinda’ yapata umaarufu wa kipekee lakini mtunzi amesalia maskini

SIMON CIURI NA WANGU KANURI

Mshairi wa mapenzi, Percy Bysshe Shelley, katika shairi lake ‘To a Skylark,’ lililochapishwa mwaka wa 1820 alisema kuwa nyimbo tunazopenda mahadhi yake sana ndizo huzungumzia mawazo yetu yenye machungu. Kauli hii bado ni kweli karne moja baadaye.

Baada ya miaka 36, Dickson Njoroge mwenye umri wa miaka 69 na mtunzi wa wimbo uliovunja kinga za umaarufu kwa jina ‘Firirinda,’ amepata kutambulika katika ngazi ya kitaifa. Ukweli ni kwamba, umaarufu kwa mtunzi yeyote ni mzuri lakini wakati ambapo umaarufu huu unakufikia na mahitaji mengi ya kifedha, unahuzunisha.

Wimbo huu wa ‘Firirinda’ sasa upo kinywani mwa Wakenya wengi lakini Njoroge ambaye kwa jina la usanii anafahamika kama Dik Munyonyi, ana mawazo machungu na mikosi.

Firirnda ni wimbo wenye kuonyesha uchangamfu katika kuwakaribisha wageni kwa njia ya Kiafrika kwa kuunganisha utamaduni na ukarimu.

Mchango wa kugharamia matibabu ya kiafya

Taifa Leo Dijitali ilipatana naye Dickson katika uwanja wa Icons, wakati ambapo alikuwa akihudhuria mchango wa kugharamia matibabu yake ya kiafya baada ya kulazwa hospitalini mara nyingi kisa ugonjwa wa moyo.

“Maisha yangu ya kifedha hayajabadilika hata ingawa wimbo wa ‘Firirinda’ unachezwa kila mahali. Ndio nimefahamika lakini kifedha hali ni ile ile. Bado mimi ni masikini,” akasema Munyonyi ambaye alipoteza sauti yake miaka michache baada ya kuutoa wimbo ‘Firirinda’ mwaka wa 1986.

Anazungumza kwa sauti iliyopwelea hivi sasa na hali hii huzidi wakati anapoelekea River Road, pale ambapo safari yake ya uimbaji ilianza.

“Hali hii huzidi nikijongea River Road. Sijawahi kuelewa mbona hii hutendeka. Kupoteza sauti yangu kumekuwa mojawapo ya nyakati zenye uhafifu sana maishani mwangu,” alisema.

Mchango huu wa kifedha wa kugharamia matibabu yake ulihudhuriwa na mkurugenzi wa bodi ya filamu na uanishaji (KFCB) Ezekiel Mutua na waimbaji wa Kenya wengi ambao walitoka maeneo ya mlima Kenya.

Tueneze maandishi yenye ubunifu

KFCB imejiunga na mwenyekiti wa chama cha Tamco (Talented Musicians and Composers) Ephah Maina katika kupendekeza ‘Firirinda’ kama njia ya shirika lake la kueneza maandishi ya ubunifu.

“Tutamuunga mkono katika kuuzindua upya wimbo huo. Tumeelezwa na madaktari kuwa baada ya mwezi mmoja, Munyoyi ataweza kuzungumza vizuri na kupona sauti. Mawazo yetu ni kugeuza talanta yake kuwa pesa kupitia maandishi safi na kuhakikisha kuwa Firirnda imejulikana zaidi kuliko vile wimbo wa Jerusalema ulijulikana na pia kwa wakati huo kupigana na uharamia,” akasema bw Mutua.

Wimbo wa ‘Firirinda’ na ‘Munyonyi’ ulitayarishwa na Talanta Promotions. Cha kushangaza ni kuwa ‘Munyonyi’ ulivuma haraka sana, ukamfanya kufahamika na kubadilisha nyota yake ya bahati.

“Firirnda haukufanya vizuri kwenye soko wakati huo. Haukukubaliwa. Munyonyi ulifahamika sana kiasi cha kwamba katika kila tamasha, nilikuwa mwanamuziki wa mwisho kutumbuiza umati,” akaeleza Munyonyi ambaye alianza kazi ya muziki mwaka wa 1971.

Kama wasemao husema, kila kitu na wakati wake. Zaidi ya miongo mitatu baadaye, ‘Firirinda’ imerejea tena kwa mpigo. Umaarufu wake ulikolea wakati ambapo mtangazaji wa redio ya Inooro, Jeff Kuria, alichapisha katika mtandao wa kijamii wa vijana wa TikTok.

Hata kabla ya wiki kumalizika, wimbo huu ulizivunja kingo za umaarufu haswa katika stesheni za redio za lugha ya mama. Katika shamrashamra za kifamilia na vituo vya kujiburudisha haswa sehemu za kati ya Kenya, midundo ya kingoma ya wimbo huu wa ‘Firirinda’ ulisikika huku ukiwaleta pamoja wazee kwa vijana, wake kwa waume bila kuzingatia madaraja ya kijamii.

Utamaduni wa Kiafrika

“Wimbo huu unaonyesha ukarimu wa utamaduni wa Kiafirka haswa wakati wa kuwakaribisha wageni katika shamrashamra za kijamii na kitamaduni. Wakenya ni watu wazuri, wanawapenda wageni. Wimbo huu unasherehekea utajiri wa utamaduni wa Kiafirka,” akasema Munyonyi.

Hivi, una watoto wowote waliojiunga na muziki?

“Nilikuwa na watoto nane lakini wawili wamekwisha aga. Ni mmoja tu, Munyonyi Junior, ambaye ameonyesha kuwa na hamu ya muziki. Tangu nipoteze sauti yangu, mimi daima hujitumbuiza pamoja na mwanangu ambaye huimba nikicheza gitaa. Tumerekodi albamu na wimbo mmoja unamlenga rais,” akasema.

Bw Maina alisema kuwa wanachama 500 wa Tamco wametoa kiasi kizuri cha pesa ili kufidia matibabu ya bw Munyonyi katika hospitali ya Nairobi.

“Chini ya chama cha Tamco, tunamradi ambao tunatumia katika kufidia matibabu ya kiafya ya Munyonyi. Ombi letu kwa serikali ni kuwa watu ambao hutumia muziki wetu kujichumia riziki wanapaswa kulipa mwanzoni wakati wa kupata leseni ili watunzi waweze kufaidika,” akasema bw Maina.

Chama cha Tamco aghalabu kimejumuishwa na wanamuziki kutoka sehemu za mlima Kenya. Wamezindua chaneli ya YouTube na msimbo wa Skiza Tune wa ‘Firirnda’ ili Munyoyi aweze kupata mapato kupitia muziki wake, hata ingawa imepita miongo mitatu.

You can share this post!

Umetuvunjia heshima, wasusi wamfokea Boniface Mwangi

Seneti yapinga mbinu ya serikali kusaka mgao wa Sh370...