Michezo

Firmino, Mane wang’aa gozi la Brazil na Senegal

October 11th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

IDARA ya ushambuliaji ya Liverpool ilitoa nyota wa mechi ya kirafiki huku Brazil ikikabwa 1-1 na Senegal mnamo Alhamisi uwanjani National Stadium, Singapore.

Brazil haina mechi ya kushindania alama hadi Machi mwaka ujao itakapoanza kampeni yake ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la mwaka 2022.

Hata hivyo, mabingwa hawa wapya wa soka ya Copa America wako makini kuingia kampeni hiyo wakiwa wamejiandaa kisawasawa na walielekea nchini Singapore juma hili kwa mechi mbili za kujipima nguvu.

Mabingwa hawa mara tano wa dunia watakabana koo na Super Eagles ya Nigeria hapo Jumapili.

Walianza ziara ya Singapore dhidi ya Teranga Lions ya Senegal iliyofika fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) miezi mitatu iliyopita.

Brazil ilionekana itafanya Senegal kuwa kitoweo ilipochukua uongozi uongozi dakika ya tisa.

Mvamizi matata wa Manchester City, Gabriel Jesus alishambulia kutoka pembeni kulia na kisha kuvutia Firmino krosi safi. Firmino alikamilisha shambulio hilo kwa ustadi na kufikisha mabao yake ya kimataifa kuwa 13.

Hata hivyo, mshambuliaji mwenzake kutoka Liverpool, Sadio Mane hakuwa tayari kusalimu amri kwa urahisi katika mechi hiyo muhimu iliyopeperushwa na Apu rasmi ya timu hiyo kwa mashabiki wa Liverpool.

Mshambuliaji wa Bristol City, Famara Diedhiou alisawazisha 1-1 baada ya kufuma penalti safi kabla ya timu hizi kuenda mapumzikoni na hakuna mabao zaidi yalishuhudiwa katika dakika 45 za mwisho, huku joto na uwanja mbovu ukiathiri mchezo.

Mechi tatu bila ushindi

Hata hivyo, hiyo haitakuwa sababu tosha kwa Brazil, ambayo sasa haina ushindi katika mechi tatu na ingetamani sana kusherehekea mechi ya 100 ya Neymar kwa ushindi.

Mshambuliaji huyo wa Paris Saint-Germain alikaribia sana kupata bao aliposukuma kombora katika kipindi cha pili lililoguswa na kuenda nje. Naye Mane aligonga mlingoti alipopiga shuti kutoka nje ya kisanduku zikisalia dakika tano kipenga cha mwisho kilie, huku timu hizi zikiridhika na sare mbali na nyumbani.

Kwingineko, mabingwa wa Afrika Algeria walikabwa 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mjini Blida nayo Gabon ikazima Burkina Faso jijini Paris, Ufaransa.