Dondoo

Fisi afunzwa adabu kwa kutamani visivyolika

March 27th, 2018 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

KITUNDU, MBOONI

KALAMENI mmoja wa hapa alijipata kona mbaya alipofumaniwa akitongoza mke wa jirani yake plotini. Inasemekana jamaa huyo hakuwa ameoa na alipenda kutongoza  wake za watu.

Kilichoshangaza wengi ni kuwa jamaa huyo hakuwa akitongoza mabinti ambao hawajaolewa. “Alikuwa akilenga wake za watu na hakuwa akiona haya. Kwake, huo ulikuwa uraibu,” alieleza mdokezi.

Siku ya kioja, jamaa alionekana na wakazi akiandamana na mke wa rafiki yake plotini huku akimrushia mistari ya mapenzi. Ni katika hali hiyo mume wa mwanamke huyo alipofahamishwa na wenzake kuwa mke wake alikuwa akiwindwa na jamaa huyo.

“Jirani mmoja aliamua kumpigia simu mume wa mwanamke huyo alipomuona akiandamana na jamaa hadi kwake,” alisema mdokezi.

Bila kupoteza muda jamaa alienda katika ploti hiyo kujua kilichokuwa kikiendelea. Penyenye zinasema jamaa alipata mwenzake akiendelea kujitetea kutoka kwa mke wake na hapo akachemka na kuanza kumfokea.

“Unafanya nini na mke wangu. Yaani umeamua kutongoza wake za watu ilhali kuna mabinti chungu nzima mitaani.

Bure kabisa wewe. Badala ya kutafuta mabinti ambao hawajaolewa unaendelea kutuharibia wake zetu. Umerogwa ama umepagawa? Tuheshimiane ama nichukue hatua mara moja,” jamaa alifoka.

Licha ya kufumaniwa peupe, jamaa alianza kujitetea lakini alizimwa kwa kuangushiwa kofi moto la usoni. “Hauna hata aibu kufungua mdomo wako kujitetea ilhali nimekupata peupe, mwehu wewe,” jamaa alikemewa huku akiangushiwa kipingo.

Kulingana na mdokezi, wanawake katika ploti hiyo na zilizo karibu walifurahi kusikia jamaa alikuwa ameadhibiwa wakisema alikuwa akiwasumbua kwa kuwataka wamgawie uroda.

…WAZO BONZO…