Fisi aibiwa tairi akila vya haramu

Fisi aibiwa tairi akila vya haramu

Na TOBBIE WEKESA

ROYSAMBU, Nairobi

KIZAAZAA kilizuka eneo hili polo alipokatiziwa raha ya kuchovya asali katika chumba cha mpenzi wake baada ya gari lake kung’olewa magurudumu.

Inasemekana gari la polo liling’olewa magurudumu dakika chache baada ya kuliegesha kando ya barabara iliyopita karibu na duka moja.

Kulingana na mdokezi, mwenye duka aliamua kung’oa magurudumu ya gari akidai kwamba polo alikuwa na mazoea ya kuegesha gari lake mbele ya biashara yake na kuelekea kwa chumba cha mpenzi wake.

“Huyu kijana amenizoea sana. Kila wakati akija kumuona mrembo wake lazima aegeshe gari lake hapa. Haoni kwamba anaathiri biashara yangu,” mwenye duka alifoka huku akielekea kulikokuwa gari.

Duru zinasema wengi walilifahamu gari hilo pamoja na mwenyewe.

“Mwenye hili gari yuko tu katika chumba kimoja sehemu hii. Lazima anakula mali yake polepole. Hatatoka saa hizi,” jamaa mmoja alisikika akisema.

Habari zilizotufikia zinasema mwenye duka alianza kung’oa magurudumu huku majirani zake wakimshangilia.

“Ng’oa magurudumu yote. Anaturingia hapa kana kwamba sisi hatuwezi kununua V8,” sauti zilisikika zikisema.

Inadaiwa kelele hizo zilimfanya polo kusitisha shughuli nzima ya kurina asali na kuteremka kubaini kilichokuwa kikiendelea.

Alipigwa na butwaa kupata watu wamelizingira gari lake bila magurudumu mawili ya mbele.

“Mwenyewe ndiye huyu hapa. Bosi leo lazima utatembea kwa miguu hadi kwako,” polo alifokewa.

Inasemekana polo aliwaka kwa hasira akimlaumu mwenye duka kwa kucheza na gari lake la pesa nyingi.

“Sijaegesha gari kwako. Liko katika egesho la umma na hata kama lingekuwa kwako, hauna ruhusa la kufanya hivi. Utalipia ujinga wako,” jamaa alisema na kutisha kuwaita maafisa wa polisi. Alilipa baadhi ya vijana kurudisha magurudumu na akaondoka.

You can share this post!

Kwake, fursa ya kumsalimia Mzee Jomo Kenyatta ilikuwa ni ya...

KINA CHA FIKIRA: Asilan usimchape na kumtesa punda...