Habari Mseto

Fisi waliolishwa sumu wavamia wakazi

December 1st, 2018 1 min read

NA BRUHAN MAKONG

KUONGEZEKA kwa visa vya fisi kuvamia wakazi katika kaunti ya Wajir kumechangiwa na hali ya wanyama hao kutiliwa sumu na kuwafanya kuchukulia binadamu kama adui, badala ya kuvamia wanyama wenzao, wataalamu wamesema.

Afisa katika mbuga ya Northern Conservation Area alisema kutiliwa sumu kwa wanyama hao kumebadili tabia yao, huku visa vya wakazi kuvamiwa, kujeruhiwa na kuuawa vikizidi kuongezeka.

Jumatatu, wakazi wanne walijeruhiwa vibaya baada ya fisi waliotoroka mbugani kuvamia vijiji viwili eneo la Wajir Kaskazini, akiwemo mzee wa miaka 70 ambaye aliumwa mara 20.

Watu wengi wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa na wanyama hao katika maeneo tofauti ya kaunti, chifu wa eneo hilo Abdicator Omar Dayib akisema licha ya wakazi kuwa na mifugo, wanyama hao wanalenga binadamu tu.

“Si kawaida kwa fisi kuvamia binadamu lakini baada ya kuchunguza tulibaini ni watu waliochangia kwa kutilia sumu mifugo nao fisi wanapokula wanaanza kuwavamia watu badala ya mifugo,” akasema.