Makala

FITTY BLACKBOY: Analenga kufikia kiwango chake Burna Boy

December 6th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

BAADA ya kukaa kimya ndani ya miaka minne iliyopita msanii ya kizazi kipya, Vincent Olsatima Athienta amerejea tena raundi hii akipania kutimiza azimio lake katika jukwaa la muziki wa burudani.

Mwanamuziki huyu ambayo kwa jina la msimbo anajulikana kama Fitty Blackboy amepania kuzamia utunzi wa nyimbo zake anakolenga kufikia hadhi ya kimataifa.

”Bila kujipigia debe ninaamini Mungu amenibariki kwa kipaji cha utunzi wa nyimbo za kizazi kipya,” alisema na kuongeza kwamba licha ya kutopiga hatua kipindi kilichopita ana imani muda wake wa kutamba utakapotimia hakuna atakayezuia.

BEDROOM

Ingawa janga la corona limezuia wanamuziki wengi kutofanya shoo zozote, ndani ya kipindi hicho anajivunia kurekodi na kuachia fataki tano. Msanii huyu ambaye hughani teke zake kwa mtindo wa Hip Hop (Swahili rap) anajivunia kuachia nyimbo kama: ‘Wikendi’ aliyoshirikisha Chris Kanya, ‘Bedroom’ (Cover) ya Harmonize aliyomshirikisha Javic Shamba.

Akishiriana na Unknown ameachia nyimbo kwa jina ‘Leo,’ bila kuweka katika kaburi la sahau teke inayozidi kutamba kwenye mitandao ya kijamii ‘Fikra’ aliyomshirikisha Jubai. Nyimbo hizo zote zimerekodiwa Wavelab Records mjini Bungoma. Anadokeza kuwa fataki hiyo imepokelewa vizuri na wafuasi wake maana ndani ya miezi miwili sasa imepata watazamaji zaidi ya 2,000.

Msanii wa kizazi kipya, Vincent Olsatima Athienta almaarufu Fitty Blackboy.  Picha/ John Kimwere

NIONYESHE NJIA

Kando na nyimbo hiyo anajivunia teke zingine kama: ‘Ndani ya fani,’ na ‘Nionyeshe Njia’ iliyopata mpenyo na kupeperushwa kupitia Televisheni ya KBC. Anasema hatua hiyo ilimtia motisha zaidi katika sekta ya muziki wa burudani. Kwa wasanii wa humu nchini analenga kifikia kiwango cha Jones Khaligraph aliyetunga vibao nyingi tu ikiwamo ‘Leave me alone,’ na ‘Gwala,’ aliyoshirikisha Ycee. Afrika analenga kukaza buti ili kutinga upeo wa msanii maarufu kwa jina Burna Boy mzawa wa Nigeria.

Kwa muziki wa Bongo anasema hupangawishwa na fataki zake msanii Fid Q hasa teke zake ‘Propaganda,’ ‘Sihitaji marafiki,’ pia hupendezwa na teke ‘Najiona mimi,’ ‘Niaje ni vipi’ utunzi wake Joh Makini.

CHANGAMOTO

Je, pandashuka gani ambazo msanii huyu hukutana nazo? “Hakika kazi ya muziki si lele mama. Mambo sio mteremko, ni tofauti kabisa na jinsi watu hudhania, gharama za kurekodi pia kuzitafutia soko nyimbo za muziki wako ni ikwazo kikubwa kwa wasanii wengi hasa wale hawajapata miziki,” anasema. Aidha anaghadhabishwa na mtindo wa baadhi ya vituo vya redio na televisheni kucheza muziki wa kigeni zaidi katika vipindi vyao.

Katika mtazamo huo anatoa wito kwa MaDJ kuzipatia nyimbo za wasanii wa nyumbani kipau mbele. Pia anawataka wasanii wa kike ambao wanaonekana kuvamia jukwaa la burudani kwa fujo kutokufa moyo bali wakaze buti na kuamini wanaweza. Katika mpango mzima anasema bado hakuna analojivunia katika muziki lakini amejifuza mengi kimuziki na kimaisha. Katika miaka mitano ijayo anasema anataka kuwa msanii wa kuigwa na wengi wanaume kwa wanawake.