Michezo

FKF, FIFA waafikiana jinsi Amrouche atakavyolipwa zaidi ya Sh109 milioni

May 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

HARAMBEE Stars sasa watashiriki mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar baada ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuafikiana na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuhusu jinsi ambavyo zaidi ya Sh109 milioni zinazodaiwa na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya, Adel Amrouche, zitalipwa.

Mwishoni mwa wiki jana, Nick Mwendwa ambaye ni Rais wa FKF, alisisitiza kwamba Kenya imeepuka adhabu kali ya FIFA ambayo vinginevyo, ingeshuhudia Harambee Stars wakitupwa nje ya michuano hiyo ya kuwania tiketi ya kuelekea Qatar.

Awali, FIFA ilitarajiwa kuelekeza fedha za maendeleo ya soka ambazo Kenya hupokezwa kila mwaka kumlipa Amrouche; kocha mzawa wa Ubelgiji na raia wa Algeria ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Botswana.

FIFA iliwahi kuwapiga Zimbabwe marufuku ya kushiriki mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi kwa kosa la kukiuka masharti ya kandarasi na kumnyima haki mkufunzi mzawa wa Brazil, Jose Claudinei ‘Valinhos’ Georgino walipompiga kalamu mnamo Machi 2015.

Chini ya kocha Francis Kimanzi, Harambee Stars kwa sasa wamo katika Kundi E pamoja na Mali, Uganda na Rwanda katika juhudi za kufuzu kwa fainali zijazo za 2022. Mshindi wa kila kundi ndiye anayefaulu kusonga mbele kwa hatua zaidi za mchujo.

Hakikisho la Mwendwa kwamba Kenya itakuwa sehemu ya vikosi vitakavyowania fursa ya kunogesha fainali zijazo za Kombe la Dunia linajiri wakati ambapo wakufunzi wengine wa zamani wa Harambee Stars, Sebastien Migne na Bobby Williamson wametishia kushtaki FKF kwa kutotii agizo la FIFA la kulipa fidia zao.

Williamson, 58, anadai FKF kima cha Sh55 milioni huku Migne ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Equatorial Guinea akidai Sh6 milioni. Wawili hao walifurushwa ghafla na FKF kinyume na maagano katika kandarasi walizotia saini.

Jopo Huru la Mizozo ya Spoti katika FIFA, liliamrisha FKF kumfidia Amrouche, 52, kima cha Sh108,194,863, mnamo Septemba 2019. Agizo jingine la kumlipa Amrouche Sh1,181,511 za ziada lilitolewa mnamo Disemba 2019 na kufikisha jumla ya fedha ambazo mkufunzi huyo anastahili kupokezwa kuwa Sh109,376,374.

FKF ambayo pia ilipigwa faini ya Sh3,243,241 iliadhibiwa kwa kosa la kukiuka masharti ya mkataba wa Amrouche alipotimuliwa kambini mwa Stars mnamo Agosti 2014.

Malipo hayo yalikuwa yawe yametolewa kufikia Aprili 23, 2020 kabla ya muda wa takriban mwezi mmoja kuongezwa.