Michezo

FKF Nairobi West ndani ya fainali Chapa Dimba

April 14th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU nne sasa ziko tayari kuwakilisha Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF) Tawi la Nairobi West katika fainali za Chapa Dimba na Safaricom Season Two, Nairobi.

Fainali za kipute hicho zitashirikisha mabingwa wa tawi la Nairobi West na Nairobi East kitengo cha wavulana na wasichana.

Kwa wavulana South B United na Uweza FC zilitwaa tiketi hiyo baada ya kushinda Vapor Sports na Kangemi Patriots mtawalia kwenye fainali za eneo hilo zilizopigiwa katika uwanja wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

WASICHANA wa Dagoretti Mixed walioshinda Beijing Rainders kwa mabao 5-4 na kufuzu kushiriki fainali za kuwania ubingwa wa Mkoa wa Nairobi katika kipute cha Chapa Dimba na Safaricom Season Two msimu huu. Picha/ John Kimwere

Nao wasichana wa Carolina for Kibera walitandika Kangemi Ladies huku Dagoretti Mixed ikizima Beijing Rainders iliyopigiwa chapuo kunasa tiketi hiyo.

Uweza FC ya kocha, Charles ‘Stam’ Kaindi ilinyamazisha Kangemi Patriots kwa magoli 5-3 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kuagana sare tasa katika muda wa kawaida.

Uweza FC ilishiriki ngarambe hiyo baada ya kunasa ubingwa wa kipute hicho Kanda ya Lang’ata. Naye kocha, John Mandela aliongoza South B United kunyamazisha Vapor Sports kwa mabao 5-3 kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 kwenye mchezo wa kusisimua.

AFISA wa Vapor Sports akizungumza na wavulana hao walipokabili South B United kwenye nusu fainali ya Chapa Dimba na Safaricom Season Two Tawi la Nairobi West Ugani KNH, Nairobi. South B United ilishinda kwa mabao 5-3 baada ya kutoka sare ya bao 1-1. Picha/ John Kimwere

Kitengo cha wasichana, Cynthia Akinyi alitikisa wavu mara moja na kubeba Carolina for Kibera na kuzoa ufanisi wa bao 1-0 mbele ya Kangemi Ladies.

”Nashukuru wasichana wangu kwa ushindi huo na kufuzu kushiriki fainali za Mkoa wa Nairobi msimu huu,” kocha wa Carolina for Kibera,Dennis Odhiambo alisema.

Nao vigoli wa Dagoretti Mixed ya kocha, Joseph Orao walilaza Beijing Raiders mabao 5-4 baada ya kutoka sare ya bao 1-1. Dagoretti Mixed ilibeba tiketi ya fainali za Tawi hilo ilipozoa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Misericordia Queens.