Habari Mseto

FKF sasa kuendesha Ligi Kuu ya Soka ya Kenya baada ya mkataba wa KPL kutamatika

September 25th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) sasa litakuwa mwendeshaji rasmi wa Ligi Kuu ya humu nchini kuanzia msimu ujao wa 2020-21.

Hii ni baada ya mkataba wa kampuni ya KPL iliyokuwa ikisimamia kivumbi hicho tangu 2003 kutamatika rasmi na Rais wa FKF, Nick Mwendwa kuthibitisha kwamba hawatarefusha kandarasi ya kampuni hiyo.

Katika kipindi cha takriban miaka 17 iliyopita, pameshuhudiwa mizozo ya mara kwa mara kati ya FKF na KPL, kilele cha kutofuatiana kwao kukiishia kwa suluhu kutafutwa mahakamani mara kwa mara – jambo ambalo Mwendwa ameshikilia kwamba limekuwa likiathiri makuzi na maendeleo ya soka ya Kenya.

Kwa mujibu wa kandarasi ya 2015, KPL walikuwa na mamlaka ya kusimamia uendeshaji wa Ligi Kuu hadi Septemba 24, 2020. Hata hivyo, KPL hawakuweza kukamilisha muda huo baada ya janga la corona kuvuruga kampeni za msimu wa 2019-20 uliosimamishwa na FKF mwishoni mwa Aprili 2020.

“Uhusiano kati ya FKF na KPL umetamatika. Wamekamilisha awamu yao ya kusimamia ligi na hatutarefusha mkataba. Sasa Ligi Kuu ya humu nchini itaendeshwa na FKF,” akasema Mwendwa.

Vita vya kibabe kati ya FKF na KPL kuhusu usimamizi wa soka ya humu nchini vilianza miaka minne iliyopita baada ya Mwendwa kuchaguliwa kuwa rais wa FKF.

Wakati huo, Mwendwa alipendekeza kupanuliwa kwa Ligi Kuu hadi kushirikisha vikosi 18 badala ya 16. Hatua hiyo iliyopingwa vikali na KPL ilichangia kujiondoa kwa kampuni ya SuperSport waliokuwa wadhamini wa ligi na wapeperushaji wa moja kwa moja wa mechi za kipute hicho.

Uhasama huo ulifufuliwa tena na KPL mwishoni mwa Aprili 2020 baada ya Mwendwa kutamatisha msimu wa Ligi Kuu mnamo 2019-20 na kutangaza Gor Mahia kuwa mabingwa kisha kuwakweza ngazi Nairobi City Stars na Bidco United kutoka Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

Maamuzi hayo ya FKF yalipingwa vikali na KPL ambao walisisitiza kwamba ndio waliokuwa na mamlaka ya kuamua hatima ya Ligi Kuu baada ya mkurupuko wa corona.

Kwa pamoja na kikosi cha Chemelil, KPL waliwasilisha kesi ambayo mwishowe ilitupiliwa mbali na Jopo la Mizozo ya Spoti (SDT).

Kwa mujibu wa Mwendwa, Ligi Kuu ya humu nchini ambayo sasa itadhaminiwa na kampuni ya mchezo wa Kamari ya BetKing kutoka Nigeria, itajulikana kama FKFPL kuanzia msimu wa 2020-21.

Kivumbi hicho kitaanza rasmi baada ya serikali kupitia Wizara ya Michezo kuafikia na ile ya Afya kuhusu wakati mwafaka wa kurejelewa kwa shughuli za soka humu nchini.

Tayari kamati shikilizi ya wenyeviti watano wa klabu za Ligi Kuu iliyoundwa Julai 2020 inashughulikia taratibu za jinsi iliyokuwa Ligi Kuu ya KPL itakavyoendeshwa na FKF katika miaka ya usoni.

Chini ya Dan Shikanda wa AFC Leopards, kamati hiyo inawajumuisha pia wenyeviti Robert Maoga (Kariobangi Sharks), Daniel Aduda (Tusker FC), Erick Oloo (Ulinzi Stars) na Ken Ochieng (Zoo Kericho).

Kamati hiyo inatalii uwezekano wa klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu kupiga kura ya kumchagua mwenyekiti huru atakayesimamia shughuli za uendeshaji wa ligi kupitia FKFPL.

Uteuzi wa wanakamati hao watano uliidhinishwa na klabu 10 kati ya 17 za Ligi Kuu ya Kenya kupitia mkutano wa mtandaoni uliohudhuriwa na wenyeviti 16 wa vikosi vya Ligi ya KPL kwa pamoja na Mwendwa mnamo Julai 22, 2020.

Wakati wa kuzinduliwa kwa BetKing watakaodhamini Ligi Kuu ya Kenya kwa miaka mitano ijayo kwa kima cha Sh1.2 bilioni, Mwendwa alifichua mipango ya FKF kushirikiana na kampuni ya StarTimes ambayo sasa itapeperusha matangazo ya mechi katika juhudi za kurejesha hadhi ya soka ya humu nchini na kuanikia dunia vipaji vya wanasoka wa kivumbi hicho.

Pia alithibitisha kwamba mechi zote za Ligi Kuu zitapeperushwa moja kwa moja mtandaoni kupitia App ambayo itawatoza mashabiki Sh200 ili kutazama mechi yoyote chaguo lao.

“Tumekuwa tukishauriana na kampuni kadhaa kwa miezi michache iliyopita. Tumeridhishwa na ofa ya StarTimes ambao watainua pia klabu za Ligi Kuu kifedha,” akasema Mwendwa kwa kusisitiza kuwa mengi ya maafikiano kati ya FKF na StarTimes yatafichuliwa katika kipindi cha mwezi mmoja ujao.

Kwa mujibu wa Mwendwa, StarsTimes kwa sasa ndio watakaopeperusha mechi zote za Ligi Kuu ya FKFPL kwa kipindi cha miaka 10 ijayo kuanzia msimu wa 2020-21.

Maafikiano hayo kati ya FKF na StarTimes yatashuhudia vikosi vyote 18 vya Ligi Kuu ambavyo tayari vina uhakika wa kupokezwa Sh8 milioni kutoka BetKing kila msimu, sasa vikipigwa jezi zaidi kifedha.

FKF imewahakikishia wadau wa soka ya humu nchini kwamba klabu za Ligi Kuu sasa zitakuwa zikipokea jumla ya Sh12 milioni kila msimu kwa kuwa StarTimes watakuwa wakitoa Sh4 milioni zaidi kwa kila kikosi.