Michezo

FKF sasa yatishia kuondoa Harambee Stars mchujo wa Afcon

October 31st, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) limetishia kuiondoa timu ya taifa ya Harambee Stars kwenye mchujo wa mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zitakazoandaliwa Cameroon mnamo 2021.

Kulingana na Nick Mwendwa ambaye ni Rais wa FKF, hawatakuwa na jingine la kufanya ila kuichukua hatua hiyo iwapo Serikali haitatoa fedha za kufanikisha maandalizi ya Stars kwa minajili ya kivumbi hicho kufikia Novemba 5, siku nne kabla ya tarehe ambapo timu ya taifa imeratibiwa kutua jijini Cairo, Misri.

Ilivyo, huenda Stars wakakosa mechi mbili za ufunguzi wa Kundi G dhidi ya Misri na Togo. Misri ndio waliokuwa waandalizi wa makala ya AFCON 2019 ambayo yaliwashuhudia Desert Foxes kutoka Algeria wakitawazwa mabingwa baada ya kuwazidi maarifa Senegal waliopigiwa upatu kuunyanyua ufalme wa kivumbi hicho. Zaidi ya Kenya, Misri na Togo, Comoros ndio wapinzani wengine katika Kundi G.

“FKF haina pesa kwa sasa na sioni uwezekano wa Stars kuingia kambini kujiandaa kwa mechi mbili zijazo za kufuzu kwa AFCON 2021,” akatanguliza Mwendwa.

“Tulipokeza serikali bajeti yetu mapema. Ingawa hivyo, bado hatujapokea pesa wala majibu kwa maombi yetu. Hali hii inatia hofu zaidi hasa ikizingatiwa kwamba ni takribani wiki mbili pekee zimesalia kabla ya siku ya mechi kati ya Kenya na Misri ugenini,” akaongeza kwa kusisitiza kwamba vinara wa FKF hawapo radhi kuendelea kutumia pesa zao binfasi kuendesha baadhi ya shughuli za timu ya taifa.

Kauli ya Mwendwa inatolewa saa chache baada ya kuagiza vipusa wa Harambee Starlets, kuvunja kambi iliyokuwa iwape jukwaa la kujifua kwa mechi dhidi ya Zambia katika jitihada za kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan mnamo 2020.

Upande wa kina dada

Kufikia hatua hiyo, Starlets walikuwa wamewabandua Malawi na Ghana katika raundi mbili za kwanza za mchujo.

Chini ya kocha David Ouma, Starlets wamepangiwa kuchuana na Zambia katika raundi ya tatu wiki ijayo hata ingawa dalili zote zinaashiria kuwa huenda mchuano huo usipigwe kutona na uchechefu wa fedha unaoikabili FKF.

Kwa upande wao, Stars wamepangwa kuanza kampeni za kufuzu kwa AFCON 2021 dhidi ya Pharaohs kutoka Misri mnamo Novemba jijini Cairo kabla ya kurejea Nairobi kuwa wenyeji wa Togo.