Michezo

FKF yapigwa faini kwa sababu ya Naibu Rais Ruto na Bw Odinga

December 9th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Soka Kenya (FKF) ni miongoni mwa mashirikisho saba yaliyoadhibwa vikali na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) hapo Jumanne baada ya kiuka sheria zake mwezi Novemba.

FKF imepigwa faini ya Sh1 milioni kwa kuruhusu Naibu Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwa kuingia katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani ghafla na kwa vishindo.

Viongozi hao wawili waliingia uwanjani kuzungumza na timu ya Harambee Stars wakati wa mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Bara Afrika (AFCON) dhidi ya Comoros mnamo Novemba 11.

“Walikuwa na maafisa wengi wa usalama na kupuuza maafisa wetu wa usalama waliokuwa wameajiriwa na CAF,” CAF ilieleza kosa la FKF ikitoa adhabu hiyo.

Wakati wa mechi hiyo ya mkondo wa kwanza ya Kundi G, Youssouf M’Changama aliweka wanavisiwa wa Comoros kifua mbele dakika ya 26 kabla ya mshambuliaji wa JS Kabylie Masud Juma kusawazishia Kenya dakika ya 65.

Harambee Stars ya kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee ilichapwa 2-1 katika mechi ya marudiano mjini Moroni na sasa ina nafasi finyu ya kuwa nchini Cameroon mwaka 2022 kwa dimba la AFCON.

Inashikilia nafasi ya tatu kwa alama tatu, huku Misri na Comoros zikiwa sako kwa bako katika nafasi mbili za kwanza kwa alama nane. Togo imeshabanduliwa kwa kuambulia alama moja kutokana na michuano minne ya kwanza. Mechi mbili za mwisho za kundi hili zitasakatwa Machi 2021, huku timu mbili za kwanza zikijikatia tiketi kushiriki AFCON mapema mwaka 2022.

Mataifa mengine yaliyoadhibiwa na CAF ni Gambia kwa kutodumisha uanaspoti ilipofanya timu ya Gabon kulala sakafuni katika uwanja wa ndege kabla ya mechi ya kuingia AFCON ya kundi D. Kwa kosa hilo, Gambia ilipigwa faini ya Sh10 milioni. Italipa Sh5 milioni pekee. Itahitajika kulipa Sh5 milioni ikirudia kosa hilo chini ya miezi 24 ijayo.

Mshambuliaji wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang pia alifanya timu yake ya Gabon kupigwa faini ya Sh1 milioni baada ya kutoa matamshi kuhusu walivyotendewa Gambia yaliyoonekana kuchafulia CAF sifa.

Kocha wa Sudan, Mfaransa Hubert Velud alisababisha taifa hiyo kupigwa faini ya Sh1 milioni baada ya kuingia uwanjani kulalamikia timu yake kunyimwa penalti wakati wa mechi ya Kundi C ya kufuzu kushiriki AFCON dhidi ya Ghana mjini Omdurman. Alimzuia pia refa ya kunyanyua kibendera na pia kudhalilisha marefa wa Afrika akidai baadhi ya maamuzi yao yamechangia katika Afrika kusalia nyuma katika kazi ya urefa.

Mauritania imepigwa faini ya Sh1 milioni kwa tabia ya mashabiki wake kusababisha moshi kuwa uwanjani wakati wa mechi ya kupigania tiketi ya AFCON ya Kundi E dhidi ya Burundi nchini Mauritania.

Burundi pia ilipokea adhabu sawa na hiyo kwa kutozingatia masharti ya CAF kuhusu idadi ya mashabiki waliohitajika kuwa uwanjani wakati huu wa janga la corona katika mechi ya marudiano jiji Bujumbura.

Vilevile, Benin ilipigwa faini ya Sh1 milioni baada ya mashabiki kutumia nguvu kuingia uwanjani wakati wa mechi ya kuingia AFCON ya Kundi L dhidi ya Lesotho.

Klabu ya Pyramids kutoka Misri ilipokea adhabu mara mbili. Mashabiki, wachezaji na maafisa wa Pyramids walisababishia klabu hiyo kupigwa faini ya Sh1 milioni waliposhambulia refa wakati wa fainali ya Kombe la Mashirikisho (Confederation Cup) dhidi ya Berkane kutoka Morocco mnamo Oktoba 25.

Mchezaji wa Pyramids Ibrahim Hassan Abdellatif amepigwa marufuku miezi 24 baada ya kupatikana ametumia dawa za kusisimua misuli wakati wa mechi ya nusu-fainali ya Confederation Cup dhidi ya Horoya Conakry kutoka Guinea. Atatumikia marufuku miezi miwili pekee kuanzia Novemba 18, 2020 hadi Januari 18, 2021 asipoparudia kosa hilo.